Kabila la Wahadzabe ni moja ya makabila yaliyopo
eneo la hifadhi ya Ngorongoro, makabila mengine ni pamoja na wamasai na
wadatoga ambapo kwa pamoja yanaguswa na mradi wa Jiopaki ya Ngorongoro maarufu kama
Ngorongoro-Lengai UNESCO Global Geopark ambayo kwa sasa imeasisi uanzishwaji wa
makumbusho kubwa na ya kisasa iliyopo Wilayani Karatu inayosimamiwa na Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Makala haya inaangazia thamani ya mnyama nyani
katika kuoa kwenye kabila la wahadzabe. Kwa mujibu wa wazee mbalimbali wa
kabila hilo, katika maisha yao ya kila siku jamii hii huishi kama kundi moja linaloshirikiana bila
utengano wa familia au ukoo tofauti na makabila mengine nchini ambayo
hutambuana pia kwa kutumia ukoo.
Wahadzabe katika jiopaki ya Ngorongoro wanapatikana
pembezoni mwa Ziwa Eyasi ambapo wameweka
maskani yao na kuendeleza maisha yao ya jadi kwa kuwinda, kurina asali na
kuchimba mizizi ambapo mfumo huo wa Maisha
yasiyobadilika yamepambwa na kila aina
ya silka, tabia na taratibu za utamaduni wa jadi.
Jambo usilolijua na la kusisimua ni kuwa kijana
anapotaka kuoa katika kabila la Wahadzabe ni lazima awe shupavu na hodari wa
kuwinda wanyama na kijana hutakiwa
kuhakikisha kuwa ana uwezo wa kukabiliana na wanyama wakali wanaoishi porini na
moja kati ya sifa za kuoa katika kabila hili ni kuhakikisha kuwa una uwezo wa
kuua wanyama wakubwa.
Kijana aliyefikisha umri wa kuoa ili akabidhiwe mke
ni lazima aue Madume mawili ya nyani, Pundamilia mmoja, Pofu mmoja na madebe
mawili ya asali ambayo ndio yanakamilisha mahari, hivyo mshenga wa kihadzabe
hutakiwa kupeleka ukweni na hapo ndipo unaweza kukubaliwa posa na kukabidhiwa
mke.
Kichwa cha nyani siku ya harusi huliwa na baba mkwe kudhihirisha kuwa hiyo ni
heshima ya baba mzaa chema ambapo hakuna mtu mwingine katika jamii hiyo
atakayeruhusiwa kula kichwa hicho na hivyo kumfanya baba mkwe kujisikia kuwa
kweli anaheshimika kwa kumuozesha binti yake kwenda familia nyingine.
Je wataka kujua zaidi? Naaam, Ulaji wa kichwa cha
Nyani kwa baba mkwe siyo siku ya Harusi tu laa hasha, kijana hukabiliwa na
mtihani wa kupeleka kichwa cha mnyama huyo kwa baba mkwe hata baada ya kuoa kwa
maana nyingine kila ndani ya nyumba anapoliwa nyani kichwa chake lazima
kipelekwe kwa baba mkwe.
Kwa kabila la wahadzabe nyani ndiyo mnyama mwenye
thamani kuliko wanyama wote hii ni
kutokana na utamu wa nyama yake ambapo
jamii hiyo huamini kuwa nyama ya Nyani ni tamu kutokana na mnyama huyo kula
matunda matamu ambayo binadamu pia anakula hivyo kuwa na nyama ambayo utamu
wake hauelezeki labda mpaka uijaribu hivyo thamani yake inakuwa kubwa
kulinganisha na Wanyama wengine ambao wanakula majani.
Kutokana na sababu hizo ndio zinaifanya jamii ya
Wahadzabe kumtumia mnyama huyo na nyama yake
katika matukio yote ya kijamii ikiwemo kupatikana kwa mtoto, harusi,
misiba na matambiko mbalimbali ya kijamii.
Dhana na imani hii ni tofauti na jamii ya waswahili
ambapo suala la ushenga huzingatia umri, hekima na kuaminika kwa mtu katika
familia inayooa. Jamii ya wahadzabe mchakato wao wa kuoa huanzia kwa
wahusika wenyewe kwa muktadha wa muoaji
na muolewaji kukubaliana kuwa wana upendo wa kweli.
Kwa jamii hii, suala la Mshenga sio muhimu sana hata
kama ana umri, hekima na busara zinazotakiwa isipokuwa kitu cha kwanza
kinachotakiwa ili uweze kupata mke katika jamii ya wahadzabe ni uwezo usiokuwa na shaka katika kulenga mshale na kuua mnyama muhimu kama
Nyani,kwa kufanya hivyo unadhihirisha kwamba wewe ni mwamba na unastahili
kupata mwari wa kihadzabe.
Kwa jamii ya
wahadzabe wanyama wakubwa wengine ambao wahadzabe huwapenda ni Kudu, Pofu
na Twiga ambapo katika jamii
hii kwa sasa kumekuwa na changamoto ya
kuwapata wanyama hao tofauti na miaka ya nyuma kutokana na sheria na taratibu
za uhifadhi wanyamapori.
Uwindaji sio tu chanzo cha chakula, bali ni uthibitisho wa ulinzi, ujasiri na uwezo wa
kuongoza familia ambapo wazee huanza
kuwachunguza vijana wanapofikia umri wa balehe na wakishajiridhisha kwamba kijana husika ni hodari kijana hupimwa
kwa kupewa mshale wenye sumu kidogo ili aweze kwenda kuwinda.
Akiwa katika mawindo yake kijana atakapomuona mnyama
mkubwa kama nyani, kumlenga na kumuua
hurudi nyumbani na kutoa taarifa kwa wazee ambapo wazee hao sasa huenda
kuangalia kama kweli kijana huyo amefanikiwa kuua mnyama huyo kutokana na
vingezo vilivyowekwa.
Katika kabila la wahadzabe ndoa ni maridhiano baina
ya watu wawili na hufanyika siku yoyote
ile baada ya masharti kutimizwa na tofauti na harusi za kisasa wao hawana siku
maalum iliyopangwa bali ni muda wowote na wakati wowote kijana muoaji
anapofanikiwa kuua mnyama ingawa ikibidi hutakiwa kufanya tendo la ndoa kabla
ya harusi kufanyika.
Tofauti na makabila mengine baada ya harusi
kufanyika kijana hukabiliwa na mtihani mwingine, nao ni kulazimika kuishi kwa
wiki moja ukweni, ukiwa ukweni wazazi wa binti huanza kukufuatilia kama kweli
wewe una sifa za mwanaume ikiwa ni pamoja na uwezo wa kutunza nyumba na kuishi
na familia.
Katika kipindi chote cha wiki moja wazazi wa binti humchungumza bwana harusi kwa
karibu ili kuona tabia, heshima na uwezo
wake wa kuishi na familia, hii ni hatua
ya ukomavu na kukubalika na iwapo wazazi wameridhika na mwenendo wa mwanaume
basi binti ndio hupelekwa ukweni na
wazazi wake.
Katika kipindi chote ambapo kijana anakuwa ukweni
ndio atakayekuwa na jukumu la kuwinda porini na kuleta chakula kwenye familia ili kuonyesha
kuwa anastahili kumchukua binti wa
kihadzabe na kwenda kuishi naye katika mji wake.
Aidha, kwa kuwa kipindi hicho cha wiki moja kijana
atakuwa anakula vizuri nyama za porini hasa nyani basi wahadzabe huamini kwamba mpaka
watakapomruhusu kurudi katika mji wake ndoa ya kijana huyo itakuwa imejibu na hapo
ndipo mwanzo wa familia mpya kuanza.
Ukitaka kujua mengi zaidi kuhusu jamii hii Karibu
makumbusho Urithi Geopark Museum.




0 Maoni