Tume ya Kuchunguza Matukio ya uvunjifu wa Amani yaliyotokea Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imetangaza rasmi kuanza kutekeleza majukumu yake makuu, ikiwemo uchunguzi wa kina wa malalamiko yaliyotolewa na wananchi.
Uchunguzi huu
unalenga kutoa mwanga juu ya matukio yaliyotokea, hususan vurugu za Oktoba 29,
na unatazamiwa kuwa hatua muhimu sana katika harakati za kujenga maridhiano na
uponyaji wa kitaifa nchini Tanzania.
Mwenyekiti wa
Tume, Jaji Othman Chande alisisitiza kwamba Tume imepewa jukumu la kisheria la
kuchunguza kwa kina kila taarifa, ushahidi, maoni, na mapendekezo
yatakayosaidia kujua ukweli. Kusudi kubwa ni kuhakikisha haki inatendeka na
kuimarisha amani nchini .
Mtazamo wa Wadau:
Kuanza kwa kazi
hiyo kumeitikiwa vyema na wadau mbalimbali. Viongozi wa dini wameelezea Tume
hiyo kama "daraja la kuunganisha" linalotoa fursa kwa wananchi
kuondoa mizigo mioyoni mwao.
"Kwa sisi
kama viongozi wa dini, ushiriki wa kila mmoja katika kutoa ukweli ni sawa na
kuweka msingi thabiti wa maridhiano. Ukweli ndio unaoweza kuponya majeraha ya
jamii" .
Wataalamu wa
sheria na siasa wanasisitiza kwamba michango kutoka kwa wananchi ni muhimu ili
Tume ifanye kazi kwa uhalali na kujiamini.
Wananchi nao
wanaona hatua hii kama fursa ya kipekee ya kuwasilisha malalamiko yao, matukio
ambayo yamekuwa yakiwaumiza, na kusaidia kufanya tume kuwa chombo cha kweli cha
jamii.
Ushiriki huu, kwa
mujibu wa wataalamu, ndio utakaofanya ripoti ya Tume iweze kukubalika na
kutekelezwa, hivyo kufungua njia ya kweli kuelekea maridhiano ya kitaifa.
Tume katika
taarifa yake inatoa wito maalum kwa kila Mtanzania anayeipenda nchi na
anayejali amani, hasa wale walioshuhudia au wana taarifa zinazohusu matukio
hayo, kujitokeza na kuwasilisha taarifa zao kwa ukweli na uwazi.
"Huu si
wakati wa woga, bali ni wakati wa uzalendo wa kusaidia Tume kufikia ukweli kwa
ajili ya mustakabali wa nchi yetu."
Taarifa
zinazopokelewa ni pamoja na nyaraka za maandishi, picha (mnato au mchoro) na
video (kama kanda ya sauti au rekodi) zinazohusu matukio ya uvunjifu wa amani,
vitendo vya kihalifu, vurugu, au ukiukwaji wa haki uliofanywa na wadau
mbalimbali.
Njia za
Kuwasilisha Taarifa:
Ili kuhakikisha
kila mwananchi anapata fursa ya kusaidia, Tume imetoa njia kadhaa za
kuwasilisha ushahidi na mawasiliano. Taarifa za kimaandishi, nyaraka, au
ushahidi unaowasilishwa kwa mkono unaweza kupelekwa kupitia Sanduku la Barua la
Tume: Tume ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya
uchaguzi mkuu oktoiba 2025, S.L.P 471, Dar es Salaam.
Kwa mawasiliano ya kielektroniki, wananchi wanaweza kutumia barua pepe kwenye anwani ya tovuti tume.uchunguzi@go.tz au barua pepe ya tume.uchunguzi@gmail.com. Aidha, Tume itapokea Ujumbe Mfupi wa Simu (SMS) au WhatsApp kupitia namba zifuatazo: 0743 040890 au 0737 305449. Mawasiliano pia yanawezekana kupitia mitandao ya kijamii, ambapo wananchi wanaweza kutuma taarifa kwa Tume kupitia tume_u-chunguzi kwenye majukwaa ya Instagram na X (Twitter).
Tume inawaomba Watanzania kutumia fursa hii muhimu ya kihistoria kusaidia kazi ya uchunguzi ili Tume iweze kukamilisha majukumu yake kwa wakati na kwa ufanisi, na hatimaye kusaidia kuleta suluhisho la kudumu kwa ajili ya umoja na maridhiano nchini

0 Maoni