Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge ameibuka mshindi wa Tuzo ya Mkurugenzi
Mtendaji Bora wa Mwaka 2025 iliyotolewa na kampuni ya Eastern Star Consulting
Group kwa ushirikiano na CEO Roundtable South Africa.
Tuzo hiyo imetolewa hivi karibuni katika Ukumbi wa
SuperDome jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla maalumu ya kuwatambua viongozi
100 bora na mahiri barani Afrika wanaotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya
jamii.
Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hizo hutolewa kwa
watendaji wanaodhihirisha ubunifu, uwajibikaji na matokeo chanya katika
utendaji wao wa kila siku.
Dkt. Kisenge ametambuliwa kwa uongozi wake thabiti
unaoweka mbele maslahi ya wananchi, hususan katika kuboresha huduma za tiba ya
moyo nchini jukumu ambalo limeifanya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuwa kitovu muhimu cha matibabu ya moyo
katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kupatikana kwa Dkt. Kisenge katika orodha ya
viongozi 100 bora Afrika ni ishara ya kutambuliwa kimataifa kwa jitihada zake
za kusimamia rasilimali, kuboresha miundombinu ya tiba na kuikuza taasisi ya
JKCI katika ngazi ya kimataifa.
Chini ya uongozi wake, JKCI imepanua wigo wa huduma
za uchunguzi na upasuaji wa moyo, huku idadi ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu
ndani ya nchi ikiongezeka kwa kasi. Huduma mpya za kitabibu zimeanzishwa,
wataalamu wa ndani wamejengewa uwezo kupitia mafunzo ya kisasa na taasisi
imeendelea kutekeleza miradi ya utafiti inayolenga kupunguza mzigo wa magonjwa
ya moyo nchini.
Baadhi ya wagonjwa wanaohudumiwa na JKCI wamepongeza
ushindi huo wakisema ni uthibitisho wa ubora wa huduma na uwajibikaji wa
uongozi wa taasisi hiyo.
"Nimekuwa nikitibiwa hapa kwa miezi kadhaa na
nimeona jinsi huduma zilivyo bora na za haraka. Kila mfanyakazi anaonekana
kujituma na kuwajali wagonjwa. Bila shaka tuzo hii anastahili kabisa kuipata
Mkurugenzi wao," alisema Asha Bakari mmoja wa wagonjwa.
Joseph Mushi anayehudumiwa na taasisi hiyo kwa muda
mrefu alisema tuzo hiyo ni fahari sio tu kwa JKCI bali pia kwa wananchi wanaonufaika
na huduma zake.
"Zamani tulisikia watu wakisafiri kwenda nje ya
nchi kutibiwa, lakini sasa huduma bora zinapatikana hapa hapa nchini. Uongozi
wa Dkt. Kisenge umeleta mageuzi makubwa," alisema.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na washiriki kutoka nchi mbalimbali
ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia, Malawi na Afrika Kusini ambapo
viongozi waliotoa mchango mkubwa katika sekta zao wametambuliwa rasmi.

0 Maoni