Wajasiriamali na
wakazi walioathirika na vurugu wametoa onyo kali, wakisema vitendo vya kuharibu
mali za watu ni uhalifu na si sehemu ya maandamano halali, na kuwataka vijana
kurejea kwenye maadili ya Taifa.
Gabriel Nalika
Laizer, mjasiriamali, alifafanua tofauti kati ya maandamano halali na uhalifu,
akisema wale waliohusika walikuwa wanafanya uhalifu wa kawaida.
“Huu ulikuwa ni
uhalifu kama uhalifu mwingine," alisema Laizer. Alieleza jinsi vurugu hiyo
ilivyosababisha wizi, ikiwemo kuondoa grili za madirisha, milango, na kuiba
spea za magari, hata baada ya tukio la moto kutokea.
"Maandamano ya
kuja kuharibu mali za watu hasa wafanyabiashara wadogo kama sisi, si maandamano
bali tunachukulia kama uhalifu mwigine," alisisitiza.
Benjamin, mkazi wa
Sanawari na mfanyabiashara, aliongeza kuwa wahusika hawakuwa na nia njema,
kwani walivunja maduka ya wafanyabiashara wasiohusika na maandamano.
"Hawa
watu wangekuwa wana nia
njema wasingefanya vurugu wengine kwa kuwavunjia maduka. Watu wengine wametumia
kama fursa kuwavunjia watu maduka yao," alisema Benjamin, akitoa wito kwa
mamlaka kuimarisha ulinzi.
Wito wa wadau hawa
kwa vijana ni kutumia njia za kistaarabu na kisheria kutoa maoni, ikiwemo
kuandika ujumbe kwenye mabango na kuepuka vitendo vyovyote vinavyohatarisha
amani na mali za Watanzania wenzao.

0 Maoni