Serikali, kupitia Wizara ya Afya
na Msemaji Mkuu wa Serikali, imelaani na kukemea vikali kitendo cha baadhi ya
watu kutengeneza na kusambaza picha na video za uongo zenye nia ya kuchochea
taharuki na hasira miongoni mwa Watanzania.
Kukemea huku kunafuatia kuonekana
kwa picha na video zinazoonyesha miili ya watu imewekwa pamoja, ambapo
watengenezaji wa picha hizo walidai kuwa tukio hilo limetokea katika Hospitali
ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Katika taarifa iliyotolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara ya Afya leo, Wizara ilikanusha
vikali uhalisi wa picha hiyo, ikifafanua kuwa video hiyo imetengenezwa na
wahalifu wenye nia ya kuichafua nchi.
“Wizara ya Afya imeona picha ya
video inayoonyesha miili ya watu ikiwa imewekwa pamoja na kueleza kwamba hapo
ni Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam. Wizara inapenda kukanusha uhalisi
wa video hiyo ambayo imetengenezwa na wahalifu wenye nia ya kuichafua nchi
yetu,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Wizara imewataka wananchi kuacha
mara moja kusambaza picha hizo kwa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja Sheria, na
imewataka Watanzania kuendelea kuziamini huduma zinazotolewa katika vituo vya
afya nchini kwa kuzingatia weledi unaojali utu na misingi ya maadili ya utabibu.
Akizungumza kuhusu tukio hili,
Msemaji Mkuu wa Serikali alisisitiza kuwa vitendo hivyo ni hatari hasa kwa
kuzingatia hali ya sasa nchini.
Kupitia taarifa yake, Msemaji
Mkuu alisema: “Kwa wakati huu ambapo Watanzania tumepitia madhira
yaliyosababishwa na vurugu za tarehe 29 Oktoba, 2025 sio busara kuchochea
taharuki kwa watu kwa kutengeneza picha zenye kutia uchungu na hasira kwa
watu.”
Alionya vikali kuwa wale
wanaofanya vitendo hivi sio tu wanachafua nchi, bali pia wanavunja Sheria za
nchi na kusababisha hofu isiyo ya lazima kwa umma na kutoa wito kwa Watanzania
wote kuacha mara moja vitendo vya kutengeneza na kusambaza habari au picha za
upotoshaji.
Aidha, aliutaka umma kuwa makini
na taarifa za uongo (fake news) zinazochochea chuki, hasira, na kuvuruga amani
ya nchi.

0 Maoni