Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Ezekiel Kamwaga, amesema kwa uwazi
kwamba hakuna sababu za msingi zinazoweza kuwafanya Watanzania kuandamana
ifikapo Oktoba 29, 2025, akibainisha kuwa hali ya kiuchumi nchini ni tulivu na
matumaini ya wananchi yako juu kutokana na mwelekeo thabiti wa Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Kamwaga alisema:“Binafsi
siamini kutatokea maandamano Oktoba 29, kwa sababu hakuna matatizo ya kiuchumi
yanayosababisha Watanzania kuandamana kama ambavyo tumeshuhudia kwa baadhi ya
mataifa jirani. Uchumi wetu uko imara, na wananchi wana imani na Serikali yao.”
Amewataka wale wanaojaribu kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha
vurugu, akiwemo Mange Kimambi anayejulikana kwa kampeni zake za uchochezi akiwa
Marekani, pamoja na Maria Sarungi anayesikika Kenya, kuacha kutumia changamoto
ndogo kama kisingizio cha kuwatumia vijana kisiasa.
Kamwaga amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa
ya maendeleo, ikiwemo kuboresha huduma za afya, elimu, ajira, na miundombinu ya
kijamii, jambo linaloleta matokeo ya moja kwa moja katika maisha ya wananchi.
Ameshauri pia Serikali kuendelea kuwasiliana kwa ukaribu zaidi na wananchi,
ikitoa mwelekeo wa maendeleo ya muda mfupi unaoonekana na kuguswa moja kwa moja
na jamii.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa uchumi, Tanzania inaendelea kudumisha
ukuaji wa Pato la Taifa kwa wastani wa zaidi ya asilimia 5.5 kwa mwaka, huku
bei za bidhaa muhimu zikiwa katika udhibiti. Hali hii inaifanya nchi kuwa mfano
wa uthabiti wa kiuchumi na kisiasa katika Afrika Mashariki.
Kauli hii ya Kamwaga ni ujumbe mzito kwa wapotoshaji wanaotafuta
umaarufu mitandaoni kwa ajenda za hofu na taharuki. Tanzania ni nchi salama,
yenye uongozi makini, na wananchi wake wanaoendelea kuchagua maendeleo badala
ya fujo.
Ukweli ni mmoja; Watanzania hawana muda wa maandamano; wana muda wa
kujenga Taifa lao.

0 Maoni