Sekta ya
Madini nchini Tanzania inaendelea kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya
kiuchumi na kijamii na sasa inajulikana kama Sekta jumuishi inayotoa nafasi
sawa kwa wote, wanaume, wanawake na vijana kushiriki kikamilifu. Wanawake
Wilayani Chunya ni ushahidi wa mabadiliko haya, wakivunja dhana ya zamani kuwa
madini ni kazi ya wanaume pekee.
Wakizungumza
na Madini Diary hivi karibuni, baadhi ya wanawake hao wameeleza jinsi
wanavyoshiriki katika kila hatua ya mnyororo wa madini: wapo wanaomiliki leseni
za uchimbaji mdogo, wachimbaji mahiri, wapondaji wa mawe na wafanyabiashara.
Wanasema shughuli hizo zimewawezesha kupata kipato, kulea familia, kuanzisha
miradi ya maendeleo na kujenga makazi bora.Ushuhuda wao unaonesha wazi kuwa
sekta ya madini inayoendeshwa kwa usawa wa kijinsia inaweza kuwa chachu ya
mabadiliko chanya kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti
wa Kikundi cha Wachimbaji Wanawake
Itumbi-Chunya Happiness Mabula anasema “Mimi kwenda chini umbali wa mita
200 kuchimba madini ni kitu cha kawaida sana kwangu na nimefanya kazi hii si
chini ya miaka 10, nina migodi yangu na
nimekua nikilipa kodi kwa Serikali kwa miaka yote na tunawasaidia vijana.
Anaongeza kwamba, kama wanawake wananufaika na shughuli za madini na hivyo
kuisaidia jamii. Licha ya mafanikio hayo anasema changamoto zipo kama kuvamiwa
maeneo yao.
Naye,
Makamu Mwenyekiti wa kikundi hicho Angela Sompo anasema, ‘’kikundi chetu
kilianza mwaka 2023 tukiwa wanawake 25, tulianza kwa kuwezeshana kwa
kuchangiana vifaa kazi kama makarasha, compressor na mpaka sasa tumekwisha
kutoa vifaa kwa wanachama 11 na vifaa hivi vimeturahisishia kazi zetu,’’ na
anaongeza, ‘’tulianza kwa kuchangishana michango ya shilingi milioni 1 kila
mwezi fedha zilizotusaidia kupata mitaji na kununua vifaa. Mbali na hayo, Angela anasema amekuwepo kwenye shughuli
hizo kwa miaka 10 sasa, anachimba kwenye leseni za mume wake ambazo umempatia
mafanikio ya kiuchumi. Angela anasifu juhudi za Serikali kusimamia bei ya
dhahabu na sasa wananufaika zaidi.
Kwa
upande wa Kikundi cha Wachimbaji wanawake kijiji cha Itumbi iliyopo kata ya
Matundasi-Chunya chenye makundi matatu ndani yake ya Wema , Mafanikio na Malkia, Makamu
Mwenyekiti wa kikundi Anna Francis anaishukuru Serikali kwa kuwapatia mashine
ya kusaga mawe ambayo wameifanya kama chanzo cha mapato kwani inakisaidia
kikundi cha kusaga mawe ya kototo kwa ajili ya shughuli za ujenzi. ‘’Tunauza
kokoto gari moja la tani 10 kwa shilingi 300,000/ pesa hizo zinaingia kwenye
mfuko wetu,". Mbali na vifaa, anaishukuru Serikali kupitia Chama Cha
Wanawake Tanzania (TAWOMA) kwa kuwapatia nafasi ya kushiriki katika mikutano na
makongamano hivyo kupata fursa ya kujifunza zaidi.
Ushiriki
wake kwenye shughuli za madini umemuwezesha kusomesha watoto, kujenga nyumba na
kuishi vizuri anasema Mariam Hussein
mmoja wa wanachama wa kikundi hicho na kuongeza," kuongezeka kwa bei ya
dhahabu kumetusaidia sana, kwa gram moja sasa tunapata shilingi hadi Laki mbili
na sitini na kusema sasa uchimbaji umebadilika
na Chunya imebadilika".
Vikundi
hivyo vitatu tayari vimekwishapatiwa
leseni moja ya uchimbaji mdogo iliyopo eneo la itumbi-Chunya bado ingawa bado
hawajaanza kuchimba.
Wanaume
wanazungumziaje ushiriki wa Wanawake?
Samwel Jeremiah Mhasibu wa Chama Cha
Wachimbaji Wadogo Wilaya ya Chunya
anasema‘’ Tunamshukuru Rais Samia kwa kuwainua wanawake, lakini Serikali
kwa kuanzisha masoko ya madini ya dhahabu kwasababu yanawainua wachimbaji wakiwemo
wanawake,". Anaiomba Serikali iwasadie wanawake kupata vifaa vya kuchimba.
Mabadiliko
Chanya kutokana na shughuli za Madini
"Kutokana
na ushiriki wa wa kina mama kwenye shughuli za madini, wameyaona mabadiliko ya
wazi Chunya."Sekta ya madini imebadilisha sana Chunya. Chunya sasa ina
majengo mazuri, kuna wawekezaji wa kila
aina, wa nyumba za biashara, makazi, kampuni za ulinzi, usambazaji wa vifaa.
Chunya hii haikuwa hivi kabla,’’ anasema Sofia Mwanauta mwanamke mchimbaji wa
madini Chunya na mmoja wa wanakikundi cha Wanawake wachimbaji Chunya .
Ombi kwa
Serikali na taasisi za fedha
Serikali itoe upendeleo kwa wanawake kwa kuwapatia leseni za kuchimba zenye madini
zilizofanyiwa tafiti ili wachimbe pasipo kubahatisha; wapatiwe elimu kuhusu
mfumo wa kuomba leseni na malipo yanayotolewa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), kuwawezesha kwa vifaa vya uchimbaji ili wasitumie nguvu kubwa kwenye
shughuli za uchimbaji na kwa taasisi za
fedha wameiomba Serikali iendelee kuzungumza na taasisi hizo ili ziweze
kulegeza masharti ya kukopa kwa Sekta ya Madini.
Pongezi
kwa Serikali
Vikundi
hivi vimeipongeza Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwasaidia kuweza
kufanya kazi zao za uchimbaji kwa uhuru, amani na utulivu. Pia, Serikali kwa
kusimamia bei ya dhahabu na kutokuwaacha nyuma wanawake. Aidha, wametoa
shukrani kwa Serikali kuwapatia karasha pamoja na kuishukuru kwa kuwahamasisha
kujiunga katika vikundi. Vilevile, wamepongeza
kwa kuanzishwa masoko ya madini na uwepo wa bei elekezi kwa kuwa
yamerahisisha biashara ya madini. Pia,
wanawake Chunya wameipongeza Ofisi Madini Chunya kwa kuwasilikiza wachimbaji na kutoa ushirikiano mzuri bila ubaguzi.
Wito kwa
Wanawake Wengine
Kutokana
na manufaa wanayoyapata, wamewaasa wanawake wengine nchini kutokuogopa
kushiriki katika shughuli za madini.
Wametoa hamasa kwa wanawake kujiunga
kwenye vikundi ili kufikiwa na huduma
kwa ajili urahisi licha ya kuwepo
mtazamo hasi kwa baadhi ya watu juu ya ushiriki wa wanawake kwenye sekta
ya madini, wanawake wachimbaji wanatoa hamasa kwa wengine ya kutokuogopa kwani
wanaweza.
#Vision
2030: Madini ni Maisha na Utajiri



0 Maoni