Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mgombea Ubunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent
Bashungwa, amewahakikishia Watanzania wote kuwa ulinzi na usalama umeimarishwa
nchi nzima, hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki kupiga kura
kuwachagua Rais, Wabunge na Madiwani bila hofu yoyote kesho, tarehe 29 Oktoba
2025.
Bashungwa ameyasema
hayo leo, tarehe 28 Oktoba 2025, wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kitaifa, ikiwa ni siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2025.
“Kesho, Oktoba 29,
hakutakuwa na shida yoyote. Vyombo vya usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo
ya Ndani, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi, vipo timamu nchi
nzima. Usalama umeimarishwa, kwa hiyo Watanzania tuende tukapige kura bila kuwa
na wasiwasi wowote. Na yeyote atakayethubutu kuvuruga amani, atakutana na
kisiki,” amesisitiza Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ametoa
wito kwa vijana kujitokeza kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, akiwataka
pia kujiepusha na vitendo au vishawishi vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani,
akisisitiza kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imebainisha fursa nyingi mahsusi
kwa ajili ya vijana.

0 Maoni