Menejimenti ya Wizara
ya Madini Oktoba 27, 2025 ilikutana na Wakuu wa Taasisi zake katika kikao
kilicholenga kupokea taarifa ya ufuatiliaji na tathmini kwa majukumu
yaliyotekelezwa na taasisi hizo katika kipindi cha Robo ya Kwanza ya Mwaka wa
Fedha 2025/26.
Taasisi zilizo chini ya
Wizara ni pamoja na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Tume ya Madini, Taasisi ya Uhamasishaji
Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) na
Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) cha jijini Arusha.
Katika taarifa iliyowasilishwa na Tume ya
Madini, ilielezwa kwamba, katika kipindi robo ya kwanza, tayari kiasi cha
shilingi bilioni 315.4 kimekusanywa ikiwa ni sawa na asilimia 105.14 ya lengo
la kukusanya shilingi 299.98 bilioni katika robo hiyo. Katika mwaka wa fedha
2025/26 Wizara imepangiwa kukusanya shilingi trilioni 1.4.
Kwa upande wa
STAMICO, pamoja na mambo mengine,
taarifa ilieleza kuwa, zoezi la kusimika mitambo ya uzalishaji wa mkaa wa
Rafiki Briquettes unaotokana na makaa ya
mawe unaozalishwa na shirika hilo hivi
karibuni itasimikwa katika mikoa ya Dodoma na Tabora. Tayari mitambo kama hiyo
inaendelea na uzalishaji wa nishati hiyo
jijini Dar es Salaam katika eneo la
Kisarawe, Pwani na Kiwira mkoani Songwe.
Aidha,
shirika hilo, lilisistiza kuhusu azma yake ya kuendeleza leseni zake za madini muhimu na
mkakati zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni hatua ya kulifanya
kuingia katika uwekezaji mkubwa.
Vilevile, ilielezwa
kuwa, katika robo ya kwanza ya mwaka 2025/26 jumla ya kilo 2,356.413
zimesafishwa katika Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals
Refinery chenye ubia na STAMICO kwa ajili ya Banki Kuu ya Tanzania. Ilielezwa
kwamba, hadi sasa kiasi cha tani 12 za dhahabu tayari zimenunuliwa na benki
hiyo kama amana kwa taifa tangu ilipoanza ununuzi rasmi wa dhahabu mwezi
Oktoba, 2024.
Pia, pamoja na masuala
mengine yaliyojadiliwa, taarifa ya GST kuhusu ununuzi wa helkopita kwa ajili ya
shughuli za utafiti wa kina wa madini nchini, ililezwa kwamba, taratibu za
manunuzi zinaendelea. Katika bajeti yake ya mwaka 2025/26, Wizara kupitia GST
iliahidi kununua helkopita ikiwa ni juhudi za kuhakikisha ifikapo mwaka 2030
angalau asilimia 50 ya nchi iwe imefanyiwa utafiti wa kina. Aidha, GST imeanza
ujenzi wa maabara kubwa nchini na ya kisasa Mkoani Dodoma na kwa ajili ya upimaji wa sampuli mbalimbali
nchini. Mara maabara hiyo itakapokamilika italeta ufanisi mkubwa katika
shughuli za upimaji sampuli.
Kwa upande wa Kituo cha
Jemolojia Tanzania (TGC) pamoja na juhudi zinazoendelea za kukiimarisha kituo
hicho kwa kujengwa miundombinu ya majengo, taarifa ya kituo ilileza kwamba,
kimefungua duka maalum la kuuza bidhaa za mapambo ya vito na usonara katika
eneo la Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha AICC, jijini Arusha. Hivyo kufanya
idadi ya maduka hayo kuwa mawili, ukijumuisha na duka lililopo uwanja wa Ndege
wa Kimataifa Kilimanjaro ( KIA).
#Vision 2030: Madini ni
Maisha na Utajiri



0 Maoni