TAWA yaomboleza kifo cha Dkt. Jane Goodall, Bingwa wa Uhifadhi wa Wanyamapori

 

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Dkt. Jane Goodall (1934–2025), mtaalamu mashuhuri wa primatolojia duniani, mlinzi wa mazingira na mtetezi wa haki za wanyamapori aliyetoa maisha yake kwa kazi ya kuwalinda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na taasisi yake, Dkt. Goodall amefariki dunia Jumatano akiwa na umri wa miaka 91. Utafiti wake wa muda mrefu kuhusu tabia na maisha ya sokwe umepanua kwa kiasi kikubwa uelewa wa dunia kuhusu hisia na tabia za wanyama.

Dkt. Goodall alijitolea kwa moyo wake wote katika kulinda sokwe na makazi yao ya asili, jambo lililowavutia na kuwahamasisha vizazi vingi vya wanaharakati wa uhifadhi kote duniani.

Maisha yake yamebeba ujumbe wa huruma, maarifa na hatua za dhati katika kulinda sayari yetu. TAWA inatambua mchango wake wa kipekee na inatoa pole za dhati kwa familia yake, Taasisi ya Jane Goodall, pamoja na jamii nzima ya wapenda wanyamapori duniani.

Urithi wake wa kipekee utaendelea kuwa dira na chachu kwa juhudi za kulinda urithi wa asili na wanyamapori wa Tanzania kwa vizazi vijavyo.

Pumzika kwa amani, Dkt. Jane Goodall.

Chapisha Maoni

0 Maoni