Tanzania
imeibuka kivutio katika Mkutano wa Tatu wa Nchi 11 zinazotekeleza Mradi wa
Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo unaoendelea mjini Maputo, Msumbiji,
baada ya kuonesha mafanikio katika uhifadhi na kuendeleza ufugaji nyuki
endelevu.
Mkutano
huo unaoratibiwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) umeanza Septemba
29 na unatarajiwa kumalizika Oktoba 3, 2025, ukiwaumisha zaidi ya washiriki 200
kutoka mashirika ya kimataifa, kikanda na kitaifa.
Tanzania
imewakilishwa na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
(TFS), Prof. Dos Santos Silayo, akiongoza timu ya wataalamu kutoka taasisi
mbalimbali.
Wengine
walioungana naye ni Mratibu wa Mradi wa Miombo, Dkt. Zainabu Bungwa (TFS),
pamoja na Dr. Deogratius Paulo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, na waratibu wa
miradi ya kimataifa wa GGWI na UNCCD – Bw. Malik Malik na Bw. Timotheo Mande.
FAO Tanzania imeshiriki kupitia Bw. Charles Tullah, Msaidizi wa Mwakilishi
Mkazi, akiambatana na Mratibu wa Programu, Bw. Jonathan Sawaya.
Katika
banda la Tanzania, zilijadiliwa mada kuhusu matumizi ya mfumo wa Honey
Traceability kusimamia mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki pamoja na nafasi
ya nyuki katika kuhifadhi misitu na kuongeza kipato cha jamii. Semina
ziliendeshwa na Mhifadhi Mwandamizi Linda Shio na Wawa Mohamed kutoka Chuo cha
Nyuki.
Prof.
Silayo alisema mafanikio yaliyowasilishwa yamechochewa na ushirikiano mpana
kati ya serikali, jamii na wadau wa kimataifa, na kwamba mazao ya nyuki
yananufaisha si serikali pekee bali pia wananchi wanaoshiriki katika uhifadhi.
“Jamii imewezeshwa kupitia ufugaji nyuki na
shughuli za uhifadhi, ndiyo maana banda la Tanzania limevutia mamia ya
washiriki,” alisema.



0 Maoni