Naibu
Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) anayesimamia Uhifadhi,
Utalii na Maendeleo ya Jamii, Joas Makwati, ameongoza kikao cha ujirani mwema
na viongozi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo, ambapo amesisitiza umuhimu
wa ushirikiano baina ya pande hizo mbili ili kujenga mazingira bora ya kazi na
kuimarisha uhifadhi.
Kikao
hicho kilichofanyika Oktoba 1, 2025, kiliwahusisha viongozi wa vijiji kutoka
wilaya za Karatu na Monduli, na kuhudhuriwa pia na Kamishna Msaidizi Mwandamizi
anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii kutoka NCAA, Bi. Gloria Bideberi, pamoja na
maafisa wengine wa mamlaka hiyo, walikubaliana kufanya kazi kwa pamoja.
Katika
mazungumzo yao, viongozi wa vijiji wa wilaya ya Karatu na Monduli waliainisha
changamoto zinazowakumba wananchi, kubwa ikiwa ni uvamizi wa wanyama pori kama
tembo na nyati katika makazi na mashamba ya wananchi, hali ambayo imesababisha
uharibifu mkubwa wa mazao na kutishia ustawi wa kaya zinazotegemea kilimo.
Akizungumza
wakati wa kikao hicho, Naibu Kamishna Makwati alieleza kuwa mbali na lengo la
kukuza ujirani mwema, majadiliano hayo yameweka msingi wa mipango ya pamoja ya
kutatua changamoto kati ya binadamu na wanyama pori.
Kwa
mujibu wa NCAA, mamlaka hiyo itaendelea na ziara katika vijiji mbalimbali
vinavyozunguka hifadhi, kwa lengo la kuimarisha mahusiano na kuwashirikisha
wananchi katika shughuli za uhifadhi na maendeleo ya jamii.



0 Maoni