WAKALA ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Pwani, wapo katika hatua za
kusitisha mikataba ya Makandarasi wawili wa kampuni ya HariCom International
Ltd na Trinity Manufacturing Services kwa kushindwa kutekeleza ujenzi wa miradi
ya miundombinu ya barabara kwa wakati.
Hayo
yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu,
Mhandisi Rogatus Mativila, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya ukaguzi
wa utekelezaji wa barabara inayofanyika Rufiji mkoani Pwani.
Amesema
usitishwaji wa mikataba kwa Makandarasi hao inatokana na kushinda zabuni pamoja
na kupewa malipo ya awali lakini wameshindwa kutekeleza mikataba yao.
"Kampuni
ya HariCom International Ltd ilipata zabuni ya ujenzi wa barabara ya
Polisi-Kirungi yenye urefu wa Km 1, ambapo walitanguliziwa kiasi cha shilingi
milioni 160 lakini mpaka sasa hawajatengeneza barabara na kutelekeza vifaa vyao
katika eneo la mradi," amesema.
Ameongeza
kuwa kampuni hiyo, mpaka kukamilika kwa mradi huo, gharama zake ingekuwa
shilingi bilioni 1 na milioni 70.
Kwa
upande wa kampuni ya TRINITY kampuni hiyo ilipatiwa malipo ya awali ya shilingi
milioni 460 toka mwaka jana mwezi Agosti na mradi ulitakiwa uwe umekamilika
mwaka huu, mwezi Novemba, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea katika mradi
huo.
Amesema
Tanzania inapenda Makandarasi wazawa washiriki katika masuala ya ukandarasi,
lakini baadhi ya wazawa wamekuwa sio waaminifu na kuchukuwa pesa na kushindwa kutekeleza
miradi kwa wakati na kutimiza mikataba kama zabuni zilivyotangazwa.
Amesema
hakuna ambaye hakusikia au kuona jinsi mvua za mwaka 2023 na 2024 jinsi
zilivyoharibu mazingira ya makazi ya watu wa Rufiji, kutokana na kuharibika kwa
makazi ya watu wa Rufiji kwa kuzingirwa na maji, ikiwamo kuharibika kwa
mashamba suluhisho la kuwanusuru wanarufiji ni kuboresha miundombinu, ambayo
itasaidia panapotokea mvua kunyesha changamoto tena zisitokee kwa jamii.
"Inasikitisha
kampuni zinamajina makubwa kuchukuwa tenda na ‘advance’ lakini kutekeleza
majukumu yao wameshindwa," amesema.
Mhandisi
Mativila amesema hatua zitachukuliwa kwa hayo makampuni yaliyoshindwa kufanya
kazi kwa wakati ikiwamo kushikilia vitu vyao ambavyo walivitanguliza katika
maeneo ya mradi.
Ameongeza
kuwa kutokana na kushindwa kutekeleza miradi hiyo, ameomba Makandarasi hao
wasipewe kazi zozote kupitia TAMISEMI.
Meneja wa
TARURA mkoa wa Pwani, Mhandisi Ibrahimu Kibasa amesema imefanyika juhudi za
kuwasiliana na Makandarasi hao kwa njia ya simu na wamekuwa hawapokei simu
zake.
Amesema
kuwa Kampuni ya HariCom mradi wao wa ujenzi wa barabara ya Kaunda- Kikopo yenye
urefu wa Km. 0.5 ulitakiwa kuanza toka Aprili 10 mwaka jana, lakini mpaka sasa
hakuna kinachoendelea.
Amesema
Trinity toka Agosti mwaka jana mpaka sasa pamoja na kuchukuwa pesa za ‘advance’
yeye naye hajatengeneza barabara.
Katika
ziara hiyo iliyoanza leo, baadhi ya maeneo miradi yake inaendelea kutekelezwa
na wasimamizi wameahidi watahakikisha wanaimaliza kwa wakati.
Pia
aliwataka wakazi wa Rufiji kuhakikisha wanatunza mitaro ya maji yote
iliyojengwa kwa ajili ya kupitisha maji, itumike kwa matumizi hayo na sio
kutupa taka katika mitaro hiyo.
Pia
aliitaka Halmashauri ya Rufiji kuelimisha watu juu ya usafi wa mazingira.



0 Maoni