Tume Huru
ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuwa uchaguzi mdogo wa ubunge katika
Jimbo la Fuoni, Zanzibar, pamoja na chaguzi ndogo za udiwani katika kata mbili
nchini, utafanyika Desemba 30, 2025.
Taarifa
hiyo imetolewa leo, Oktoba 3, 2025, na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa
INEC, Ramadhani Kailima, ikieleza kuwa hatua hiyo inafuatia vifo vya wagombea
waliokuwa wakiwania nafasi hizo.
Kwa
mujibu wa INEC, uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Fuoni, Wilaya ya Magharibi
B, ulisitishwa Septemba 25, 2025 kufuatia kifo cha aliyekuwa mgombea wa CCM,
Abass Ali Mwinyi.
Aidha,
chaguzi nyingine mbili za udiwani zitafanyika katika Kata ya Chamwino, Jimbo la
Morogoro Mjini, na Kata ya Mbagala Kuu, Jimbo la Mbagala, Dar es Salaam. Nazo
ziliahirishwa baada ya vifo vya wagombea waliokuwa wamepangwa kushiriki.
“Siku ya
kupiga kura kwa ubunge wa Jimbo la Fuoni na udiwani katika kata za Chamwino na
Mbagala Kuu itakuwa Jumanne, Desemba 30, 2025,” imeeleza taarifa ya INEC.
Tume hiyo
imefafanua kuwa maamuzi hayo yamezingatia masharti ya Kifungu cha 68(1), (3) na
(4) pamoja na Kifungu cha 71(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024.
Kwa
mujibu wa INEC, ratiba mpya ya uchaguzi kwa maeneo husika tayari imetolewa, na
wadau wa uchaguzi wametakiwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

0 Maoni