Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na mkandarasi
M/s STECOL Corporation ya China, kuanzia sasa watashirikiana kuyaondoa magari
yatakayokuwa yameharibika kwenye barabara ya kuanzia eneo la Mbagala Rangitatu
hadi Kongowe, ili kuepusha foleni za mara kwa mara.
Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi
Alinanuswe Kyamba amesema kuharibika kwa mara kwa mara kwa magari makubwa eneo
la mlimani na kutokana na wembemba wa barabara hiyo, na kutokuwa na mchepuko
imekuwa ikisababisha foleni kubwa na kuwa kero kwa watumiaji wa barabara hiyo
kwa nyakati za asubuhi na jioni.
“Mkandarasi wetu anayejenga hii barabara ya njiasita
kutokea Mbagala Rangitatu hadi hapa Kongowe kampuni ya M/s STECOL ya China
tumekubaliana naye tutakuwa tunaondoa magari yote yatakayokuwa yakiharibika
kwenye barabara hii, kwani ndio chanzo cha foleni kubwa na sio ujenzi
unaoendelea sasa, na hii inafanyika hata kwenye barabara nyingine magari
makubwa yakiharibika tunakwenda kuyatoa kwa kutumia mitambo au magari kuyavuta
na kuyatoa eneo la barabara,” amesema Mhandisi Kyamba.
Halikadhalika, Mha. Kyamba amesema pia TANROADS kwa
kushirikiana na mkandarasi huyo watajenga njia za mchepuko kwa kiwango cha
changarawe kwa upande wa kulia na kushoto mwa barabara kuu inayotumika sasa,
ili kuruhusu magari mengi kupita bila ya kuwa na foleni.
Pia amesema kwa nyakati za asubuhi kuanzia saa 11:00
alfajiri hadi saa 3:00 na kwa jioni kuanzia saa 11:00 hadi saa 2:00 usiku
katika eneo la daraja la Mzinga kutakuwa na askari wa usalama barabarani
watakaokuwa wakiongoza magari ili kuondoa kero ya foleni kwa madereva ambao
wanachepuka na kuziba upande mmoja wa barabara.
Mha. Kyamba amesema serikali baada ya kuona wembamba
wa barabara hii sasa inajenga njiasita kuanzia Mbagala Rangitatu hadi Kongowe
yenye urefu wa Km 3.8, kwa lengo la kuepukana na changamoto ya foleni, na
katika hizo njia mbili kila upande, na katikati barabara ya mabasi ya
mwendokasi, pia kutakuwa na njia ya watembea kwa miguu na eneo la Kibada
kutajengwa daraja la juu
Hatahivyo, ametoa wito kwa wananchi kuwa wavumilivu
katika kipindi hiki cha ujenzi na pindi ujenzi utakapokamilika basi tatizo la
foleni litakuwa historia.



0 Maoni