Serikali
ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kudumisha huduma bora kwa wazee kwa
kuhakikisha kundi hilo linapata huduma za msingi zinazowawezesha kuishi maisha
yenye heshima na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na
Makundi Maalum Dkt. John Jingu tarehe 15 Oktoba, 2025 wakati wa ziara yake
katika Makazi ya Wazee Wasiojiweza cha Tushikamane Pamoja Foundation yaliyopo
Kata ya Kwembe, Manispaa ya Ubungo mkoani Dar Es Salaam.
Dkt.
Jingu amesema wazee ni sehemu ya taifa kwakua wamelitumikia kwa muda mrefu kwa
uaminifu na kujitolea hivyo jamii ya Watanzania wana wanawajibu wa kuwasaidia
na kuwaenzi wazee kama ishara ya kuthamini mchango wao kwa maendeleo ya nchi.
“Lengo la
kuwatembelea ni kuwaona kuwajulia hali na kuendelea kuwaenzi pamoja na
kuthamini mchango wenu mkubwa katika kujenga na kuimarisha jamii yetu ya
Tanzania, ninatambua kazi nzuri inayofanywa hapa katika kutoa huduma bora, upendo
na matunzo kwa Wazee wetu," amesema Dkt. Jingu.
Aidha
amewapongeza wamiliki na waendeshaji wa makazi hayo kwa moyo wa kujitolea
wanaouonesha vilevile amewapongeza Manispaa ya Ubungo kwa usimamizi na uratibu
wa Makazi hayo jambo linaloonesha dhamira njema ya kuhakikisha wazee wanaishi
katika mazingira salama.
Kwa
upande wake Makamu Mwenyekiti Msaidizi wa Makazi ya Wazee Tushikamane Pamoja
Foundation Sada Jaha amesema changamoto kubwa katika Makazi hayo ni uhaba wa
watumishi ambao wanawahudumia wazee hao
na amewaomba wadau na Mashirika mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali
katika kuwaenzi na kuwatunza wazee hao.
“Tunamshukuru
sana Katibu Mkuu kwa kuja kutusikiliza na kutuahidi na kutuhakikishia kuwa changamoto tulizonazo zitapatiwa ufumbuzi kwa
kuwa Serikali hii ni sikivu na inawajali na kuwapa kipaumbele suala la ustawi
kwa wazee," amesisitiza Sada.
Nao
baadhi ya Wazee waliopo katika Makazi hayo wameishukuru Serikali kwa
kuwakumbuka na kuwatembelea kambini hapo ambapo kitendo hicho kinazidi kuwapa
faraja na matumaini ya kuendelea kuishi na kujiona na umuhimu kama watu
wengine.


0 Maoni