Katibu
Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hassan Abbas jana ametembelea
Hifadhi ya Taifa Mkomazi na kukagua mradi wa faru Mbula ikiwa ni moja ya ahadi
alizozitoa Septemba 30, 2025 mara baada ya kukabidhi vitendea kazi katika kituo
cha udhibiti wa wanyamapori waharibifu Goha wilayani Korogwe mkoani Tanga.
Katika
ziara hiyo Dkt. Abbas alieleza kuwa zao la utalii ni matokeo chanya ya uhifadhi
inayofanywa na maafisa na askari. Akiongea na TANAPA katika kikao kifupi Dkt.
Abbas alisema,
"Ongezeko
la Utalii ni matokeo ya Uhifadhi mnaufanya, tuzidi kushirikiana tusiishie
tulipo, twende mbali zaidi kwa kutumia rasilimali zilizopo. Tuwekeze kwenye
kujitangaza katika vivutio tulivyonavyo na siyo kujifungia ndani tukisubiri
watalii waje ndipo wajifunze kujua mazao tuliyonayo. Tuwekeze kwenye maeneo
ambayo tukiulizwa ndani ya miaka mitano au kumi ijayo ithibitishe uwekezaji
tulioufanya umeleta tija na mapinduzi ya sekta ya utalii na uchumi kwa
ujumla".
Aidha
Dkt. Abbas aliongeza kuwa Wizara kupitia
Jeshi la Uhifadhi linaendelea na mkakati
wa kukusanya fedha kupitia Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori (TWDF) pamoja na
Mfuko wa maendeleo ya utalii (TDl) itokanayo na mapato ya utalii mahifadhini na
kutolewa kwa asilimia 3% hadi 6% kuilinda mifuko hiyo kwaajili ya kukuza utalii
na uhifadhi. Pia amesema kuwa serikali imeongeza nguvu kwa kugawa vifaa na
kuboresha miundombinu ili kutatua changamoto zinazokwamisha shughuli za
uhifadhi.
Naye,
Mkuu wa Kanda ya Kaskazini Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga,
alimkaribisha Katibu Mkuu na kumshukuru kwa jitihada zote zinazofanyika kuunga
mkono maendeleo ya sekta ya uhifadhi na utalii yenye mchango mkubwa katika
ongezeko la pato la Taifa nchini.
Akiwasilisha
taarifa fupi ya Hifadhi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Emmanuel Moirana alitoa
takwimu na kuonesha kuwa Hifadhi ya Taifa Mkomazi inapiga hatua katika ongezeko
kubwa la watalii toka idadi ya watalii 489 kwa mwaka 2015/2016 na hadi kufikia
idadi ya 10991 kwa mwaka 2024/2025.
Mara
baada ya kikao hicho Dkt. Abbas alipata nafasi ya kutembelea mradi wa Faru
Mbula wenye Kilometa za mraba 13 na kujionea faru 9 kati ya 13 waliomo
katika mradi huo.




0 Maoni