Ujumbe maalum kutoka Serikali ya Uingereza, ukiongozwa na Mkurugenzi mpya wa Maendeleo wa katika Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, Bi. Anna Wilson, umetembelea Wizara ya Madini na kufanya mazungumzo na uongozi wa wizara hiyo ukiongozwa na Kaimu Kamishna wa Madini, Terrence Ngole.
Ziara hiyo
imefanyika leo Septemba 03, 2025 jijini Dodoma ambapo imelenga kumtambulisha
rasmi Bi. Wilson kwa uongozi wa Wizara ya Madini kufuatia kuanza kwake rasmi
majukumu ya kuongoza masuala ya maendeleo kutoka Serikali ya Uingereza hapa
nchini. Wakati wa kikao hicho, ujumbe huo ulipatiwa maelezo ya kina kuhusu
muundo wa Wizara ya Madini, taasisi zilizo chini yake, pamoja na majukumu ya
Idara Kuu ya Madini.
Akizungumza
katika kikao hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Madini Eng. Yahya
Samamba, Kamishna Ngole ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuendelea
kudumisha uhusiano mzuri na Serikali ya Tanzania, hususan katika kuendeleza Sekta
ya Madini.
Aidha,
Kamishna Ngole kwa niaba ya Katibu Mkuu Eng. Samamba ametumia fursa hiyo
kuiomba Serikali ya Uingereza kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali
yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta hiyo, ikiwemo: uongezaji thamani
madini nchini, kuimarisha utafiti na tafiti za kijiolojia, kuboresha
miundombinu ya maabara za kisasa, kuwezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa,
kutoa mafunzo kwa wataalamu wa ndani katika Sekta ya Madini.
“Tunatambua
na kuthamini ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Uingereza, na
tunatarajia kuendelea kushirikiana katika kukuza sekta hii muhimu kwa uchumi wa
taifa letu,” amesema Ngole.
Ngole
ameongeza kuwa moja ya mafanikio ya ushirikiano huo ni kutiwa saini kwa hati ya
makubaliano (MoU) kati ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania
(GST) na Taasisi ya Jiolojia ya Uingereza (British Geological Surrey - BGS),
inayolenga kuimarisha utafiti wa kisayansi, huduma za maabara, na kujenga uwezo
kwa watumishi wa Sekta ya Madini nchini.
Kwa upande
wake, Bi. Anna Wilson ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuwa na muundo imara wa
kiutendaji na kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kuendeleza sekta hiyo
kwa uwazi na ufanisi ambapo meahidi kuyafanyia kazi maombi yote
yaliyowasilishwa na kusisitiza dhamira ya Serikali ya Uingereza kuendelea kuwa
mshirika wa karibu wa Tanzania katika Sekta ya Madini.
“Tunaamini
kuwa kwa kushirikiana, tunaweza kufungua fursa zaidi za maendeleo endelevu
kupitia Sekta ya Madini, kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili,”
amesema Bi. Wilson.
0 Maoni