Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park iliyo chini ya usimamizi
wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA inaendelea kujidhihirisha
kama lulu mpya ya utalii nchini hususani
katika ukanda wa kaskazini, ikiwavutia wageni wa ndani na nje ya nchi kwa
mandhari yake ya kipekee na utajiri wa wingi wa idadi na spishi mbalimbali za
wanyamapori.
Leo Septemba 8, 2025 hifadhi hiyo imepokea tena kundi la
wageni wa kimataifa kutoka mataifa mbalimbali kupitia kampuni maarufu ya
utalii, Ranger Safaris & Tours, yenye makao yake jijini Arusha.
Zaidi ya wageni 20 kutoka Denmark, Australia na New Zealand
wametembelea hifadhi hiyo na kueleza kufurahishwa kwao na mandhari ya kipekee,
urithi wa kiasili na vivutio adimu vinavyopatikana hifadhini humo.
Aidha, Wageni hao
wameeleza kuridhishwa na ubora wa Makuyuni Wildlife Park na baadhi yao
wakaahidi kurejea tena Novemba mwaka huu kwa ziara ya pili.
Wakizungumza mara baada ya kutembelea hifadhi na kujionea
vivutio , wageni hao pia wameahidi kuitangaza Makuyuni Wildlife Park katika
masoko ya kimataifa, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza umaarufu na kuhamasisha
wageni zaidi kuitembelea.
Makuyuni Wildlife Park, iliyopo eneo la Makuyuni mkoani Arusha inazidi kujitokeza kama moja ya hifadhi mpya zenye fursa kubwa za kukuza utalii nchini zinazokua Kwa kasi katika viwango vya ubora wa kuwaridhisha wageni wa hadhi ya juu.
0 Maoni