Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 07, 2025 amezindua kampeni za Ubunge
jimbo la Mchinga zilizofanyika katika kijiji cha Rutamba mkoani Lindi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Majaliwa
amesema kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030 imejielekeza katika
kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kote nchini ikiwemo katika
jimbo la Mchinga.
“Katika kipindi kilichoisha Rais Dkt. Samia ameleta hapa
miradi mikubwa, ya kati na midogo, anafanya hivi kwa kutambua wananchi
wanapaswa kuhudumia, hata ilani hii imeonesha maeneo mengine yatakayotekelezwa
katika mkoa huu wa Lindi.”
Amesema kuwa Wana-Lindi wanapaswa kumchagua Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan ili aendelee kutekeleza miradi ya gesi, bandari ya uvuvi Kilwa,
ujenzi upya wa barabara ya Dar-Lindi, maboresho ya uwanja wa ndege wa Lindi,
ujenzi wa reli ya kanda ya kusini pamoja na kuunganisha mkoa wa Lindi kwenye
gridi ya Taifa ili kuwa na umeme wa uhakika.
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameleta mabilioni ya fedha kwa
ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Lindi,
ilani hii imeendelea kusheheni miradi inayokwenda kutekelezwa katika maeneo
yetu, hii ni sababu pekee ya sisi kumchagua Rais Dkt. Samia.
“Ilani ya uchaguzi ya 2025/2030 imeonesha kuwa kutaanza
kujengwa kwa kiwango cha lami barabara ya Ngongo-Ng’apa, Mandawa hadi Chikundi,
barabara hii itakuwa ni mkombozi kwa wakati wa wakazi wa maeneo haya na
itafungua uchumi kwa Wana-Lindi.”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa katika kipindi
cha miaka mitano iliyopita, Jimbo hilo limefanikiwa kuwa na magari ya wagonjwa
Manne pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ambayo kwa kiasi kikubwa
imesaidia kuboresha huduma za afya katika jimbo hilo.
“Mheshimiwa Salma Kikwete amejikita katika kuwahudumia
wananchi, kwa namna jimbo hili lilivyokaa linahitaj mtu mahiri na mwenye
dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wake, hakika Mheshimiwa Salma
ameonesha ameweza, mchagueni tena.”
Kwa Upande wake mgombea ubunge wa jimbo hilo Salma Kikwete
amesema kuwa katika katika kipindi chake amefanikiwa kushirikiana na
WanaMchinga kutafuta majibu ya changamoto yaliyo katika jimbo hilo.
“Tumepata mafanikio makubwa katika kukabiliana na changamoto
zetu, hali ilivyo leo sio sawa na tulikotoka, tumepata mafaniko katika sekta
mbalimbali ikiwemo afya, nishati, elimu, maji, miundombinu na uwezeshaji
wananchi kiuchumi, nikipata ridhaa tena tutafanya makubwa zaidi.”
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano amefanikiwa
kutekeleza mradi wa maji kutoka Ng’apa ambao utawezesha kuvifikia vijiji vingi
katika jimbo la Mchinga. “kama hiyo haitoshi tumefanikiwa kujenga zahanati,
tutaongeza juhudi za ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya.”
Naye Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha kuwa anatosha katika nafasi ya Urais, kwani katika kipindi kifupi amefanya mambo mengi tumpe nafasi aendelee.
“Alipata Urais katika wakati ambao hakutarajia, lakini amefanya
kazi nzuri, tutanufaika mara dufu, tukimpa nafasi, nimeangalia orodha ya mambo
yaliyo kwenye ilani kwa hakika amejipanga.”
Akizungumza kwa niaba ya wagombea ubunge mkoa wa Lindi, Mgombea ubunge jimbo la Mtama Nape Nnauye amesema kuwa wanakusini watamchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika mkoa huo ikiwemo utoaji wa Ruzuku ya pembejeo kwenye mazao.
0 Maoni