MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
Mwenyekiti wa Taifa , Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hawakidharau chama chochote
kinachoshiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Dkt. Samia ameyasema hayo Jumapili Septemba 7 wakati
akizungumza na umati wa wananchi huko Mlowa katika Jimbo la Mvumi Wilaya ya Chamwino
mkoani Dodoma.
Amesema: "Wanajadili huko kwa nini CCM inatumia nguvu
sana wakati upinzani haupo, waswahili wanasema ‘anayedharau mwiba ukimchoma mguu
unaota tende, sasa usisubiri mpaka uchomwe na msumari. Hapana! Hata mwiba
lazima uushughulikie".
“Kama misumari imelala, hii miiba iliyochomoza na kusimama lazima tuishughulikie ipasavyo," amefafanua mgombea huyo wa urais kwa CCM.
Alisema pia wana CCM wameridhishwa na kazi nzuri
iliyofanyika na ndio maana wamekuwa wakihudhuria kwa wingi mikutano ya kampeni.
“Wana CCM wameridhishwa na kazi iliyofanywa na ndio maana
kila tunapokanyaga kuna utitiri, watu ni wengi kwa sababu wameridhishwa na Serikali
ya Chama Cha Mapinduzi na hilo ndio jawabu kubwa zaidi kuliko yote,"
alieleza Dkt. Samia.
Akijibu maombi ya mgombea ubunge wa jimbo hilo, Livingstone
Lusinde la kuomba maji na barabara, Dkt. Samia alisema anayachukua na kwenda kuyafanyia
kazi.
Kuhusu ombi la kujengewa shule ya sekondari ya kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, amesema hilo anakwenda kulitekeleza na pia anatambua kuna kata tatu hazina kabisa sekondari nazo zitajengewa.
“Mimi kama mama, mtazamo wangu uko palepale, mama anataka
watoto washibe kwanza ndiye yeye afuate, najua nina watoto wa kulea na ninajua wana
masilahi yao lazima niyazingatie," aliongeza Dkt. Samia.
Akiwa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa katika mkutano
mkubwa wa kampeni, amesema serikali yake imejipanga kufufua na kujenga ushirika
imara kwa ajili ya kuwainua wakulima na wanaushirika nchini.
Na katika hilo, amesema vyama hivyo vitabidi vijikite katika
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kudhibiti ubadhirifu
kupitia mapato na matumizi.
Amesema serikali yake inakusudia kufufua na kujenga ushirika
imara ambao utaendesha mambo yake wenyewe ikiwamo kujipatia mikopo, kujenga
maghala na kutafuta masoko.
"Kwa usimamizi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, vyama
vya ushirika vijiendeshe vyenyewe na viwe na nguvu. Tunataka vyama vya ushirika
vifaidi nguvu ya jasho lao na kumuinua mkulima," alieleza Dkt. Samia.
Amesema serikali itahakikisha vyama hivyo vinaendeshwna na
watu mahiri na vinatumia Tehama katika hesabu zake.
Amewaahidi wafanyabiashara mjini Iringa kujenga Soko la Machinga, na tayari eneo na fedha vipo.
Na. Aboubakary Liongo -Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM
0 Maoni