Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kulifufua zao la
chai wilayani Mufindi, mkoani Iringa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mashamba yaliyotelekezwa
na wawekezaji binafsi yanarudishwa kwa vyama vya ushirika.
Akizungumza leo Septemba 6, 2025, katika mkutano wa kampeni
uliofanyika Nyororo, Dkt. Samia alisema tayari Serikali imeunda timu maalum ya
kufanya tathmini ya hali ya uwekezaji katika sekta ya chai nchini, ili kuchukua
hatua madhubuti za kulinda maslahi ya wakulima.
“Tumeamua kuwa mashamba ambayo hayajaendelezwa na
wawekezaji, yarudi kwa wananchi kupitia vyama vya ushirika. Tunataka zao la
chai lirudi kuwa chanzo kikuu cha mapato kwa Mufindi na maeneo mengine ya
Nyanda za Juu Kusini,” alisema Dkt. Samia.
Wafanyakazi wa
Kampuni ya Chai Kulipwa
Katika hatua nyingine, Dkt. Samia aligusia malalamiko ya
wafanyakazi wa Kampuni ya Chai na Kahawa ya Mufindi (Mufindi Tea and Coffee
Company) ambao wanadai zaidi ya Sh bilioni 2.7. Alisema Serikali inaratibu
mazungumzo na pande husika ili kuhakikisha wafanyakazi hao wanalipwa haki zao
stahiki.
“Tumeshapokea taarifa rasmi juu ya madai ya wafanyakazi wa
kampuni hiyo. Mazungumzo yanaendelea, na Serikali itahakikisha stahiki zao
zinalipwa,” alieleza.
Barabara za Lami,
X-ray na Huduma za Afya
Dkt. Samia pia alitangaza kuendelea kwa miradi ya
miundombinu, ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami ya Nyororo–Mtwango yenye urefu
wa kilomita 40.4 na Igowole–Kasanga–Nyigo yenye kilomita 54.5.
Aidha, aliahidi kupeleka mashine ya X-ray katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi ili kuboresha huduma za uchunguzi wa kiafya kwa wananchi wa wilaya hiyo.
0 Maoni