Wananchi zaidi ya 400 wapatiwa msaada wa nguo Kibiti

 

Zaidi ya wananchi 400 kutoka vitongoji 21 vya Kijiji cha Ruaruke, wilayani Kibiti, mkoani Pwani, wamepokea msaada wa nguo za aina mbalimbali kutoka kwa Taasisi ya Grace Mwashala Foundation, ikiwa ni jitihada za kusaidia makundi yenye uhitaji katika jamii.

Msaada huo ulihusisha vitenge vipya 200, kanzu 200, mashati 180 pamoja na nguo nyingine kama magauni, sketi, blauzi na suruali zilizopakiwa kwenye marobota 20.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Muasisi na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo, Bi. Grace Mwashala, alisema taasisi yake imekuwa ikitoa misaada kama hiyo katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuwafikia wazee, wanawake, watu wenye ulemavu, wanafunzi na wale wanaoishi katika mazingira magumu.

“Leo Grace Mwashala Foundation tumeleta msaada huu kwa wakazi wa Ruaruke ili kuwasaidia kuboresha hali zao za maisha. Nawashukuru wadau wetu, hususan Manispaa ya Kinondoni, kwa kutuunga mkono katika jitihada hizi,” alisema Bi. Mwashala.

Aliongeza kuwa msaada huo ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni ya taasisi hiyo ya kugusa maisha ya watu kupitia michango ya nguo, chakula na mahitaji mengine ya msingi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ruaruke, Bakari Ally Ntimbwi, ambaye aliratibu zoezi hilo kwa kushirikiana na wenyeviti wa vitongoji, alimshukuru Bi. Mwashala kwa moyo wake wa kujitolea na kuwasaidia wananchi wa kijiji hicho kwa mara ya pili mfululizo.

Wakazi waliofaidika na msaada huo, akiwemo Bi. Fadhila Yusuf Liyana na Bi. Fatuma Saidi Nkopi, walieleza furaha yao kwa kupokea vitenge, magauni na nguo nyingine, huku wakitoa wito kwa wadau zaidi kuiga mfano huo wa kujali jamii.

“Tunashukuru sana kwa msaada huu, umetufikia kwa wakati mzuri. Tunaomba taasisi zingine ziige mfano huu wa Grace Mwashala Foundation,” alisema Bi. Fatuma.

Nao baadhi ya wanaume waliopokea kanzu na suruali, akiwemo Habibu Bakari Mbande na Jumapili Omary Yundai, walisema msaada huo umeleta furaha majumbani mwao kwa kuwa kila mtu katika familia ameguswa.

“Leo tunaondoka hapa tukiwa na furaha. Sio sisi tu, hata wake na watoto wetu nao wamepata nguo. Asante sana Grace Mwashala Foundation,” alisema Jumapili Yundai.

Muasisi na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Grace Mwashala Foundation, Bi. Grace Mwashala akiwa anajiandaa kufungua furushi za nguo za msaada kwa ajili ya kuzigawa kwa zaidi ya wananchi 400 kutoka vitongoji 21 vya Kijiji cha Ruaruke, wilayani Kibiti, mkoani Pwani.

Muasisi na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Grace Mwashala Foundation, Bi. Grace Mwashala akiwa ashika vitenge kwa ajili ya kuvigawa kwa wakinamama wa vitongoji 21 vya Kijiji cha Ruaruke, wilayani Kibiti, mkoani Pwani.

Muasisi na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Grace Mwashala Foundation, Bi. Grace Mwashala akigawa vitenge kwa wakinamama wa vitongoji 21 vya Kijiji cha Ruaruke, wilayani Kibiti, mkoani Pwani.

Wazee wa vitongoji 21 vya Kijiji cha Ruaruke, wilayani Kibiti, mkoani Pwani wakigaiwa kanzu zilizotolewa na Taasisi ya Grace Mwashala Foundation.


Chapisha Maoni

0 Maoni