Jamii ya wamasai waliohamia katika kijiji cha Msomera kutoka
ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wameshiriki tamasha la Kitamaduni na Kimila la
Wamasai (Orkwaak le Maasae 2025), linalofanyika Wilaya ya Siha mkoani
Kilimanjaro.
Wananchi hao kutoka Msomera walihamia eneo hilo wakitokea
hifadhi ya Ngorongoro wameungana na wananchi wengine wa kabila la kimasai
kutoka maeneo mbalimbali nchini na kushiriki tamasha la Orkwaak le Maasae lenye
lengo la kudumisha na kuenzi mila,
desturi na urithi wa kitamaduni wa jamii ya Kimasai, kujifunza, kubadilishana
maarifa na kuonesha utambulisho wao wa kitamaduni.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa tamasha hilo
lililokutanisha wananchi zaidi ya 30,000 , Bi. Juliana Thadei Saidimu, mkazi wa
Msomera, amesema wanafurahi kuona kwamba wanakutana na wenzao kutoka mataifa mbalimbali
kusherekea siku hiyo.
Kwa upande wake kiongozi wa kimila kutoka Msomera, Bw. Komba
Riko Lodoo, alisema hatua ya serikali kuendelea na kushirikisha wananchi katika
matukio ya kijamii na kitamaduni ni ushahidi kuwa, hata baada ya kuhamia
Msomera, jamii hiyo bado imebaki thabiti katika kuenzi mila zao.
"Wananchi tuliotoka Ngorongoro kwenda Msomera sio kuwa
tumekuwa huru katika uzalishaji wa Uchumi, kujitegemea, kupata huduma bora za
kijamii lakini pia tunapata uhuru wa kufanya shughuli zetu za kimila kwa kuwa
maeneo tunayo lakini pia tunapata fursa adhimu kama hii kushiriki na wenzetu
kudumisha mila na tamaduni za kimasai kwa pamoja," alisema Laigwanan
Lodoo.
Kupitia tamasha hili la siku tatu, jamii hiyo ya wamasai
inaendeleza dhamira yake ya kulinda, kuhifadhi na kukuza urithi wa kitamaduni
wa makabila ya Tanzania, ili kuhakikisha thamani ya mila na desturi inabaki
kuwa urithi hai kwa Taifa.
0 Maoni