TBN yahimiza kampeni za amani uchaguzi mkuu 2025

  

Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) umetoa wito kwa vyama vya siasa, wagombea na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kampeni za uchaguzi mkuu nchini zinafanyika kwa amani, kufuata sheria na kanuni zote za uchaguzi, huku wakizingatia maslahi mapana ya taifa. 

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, imesema kuwa utunzaji wa amani na utulivu wa taifa ni jukumu la kila mmoja, na kwamba kipindi cha kampeni ni muda muafaka kwa vyama kueleza sera na ilani zao kwa njia ya kistaarabu bila kuibua taharuki au chokochoko. 

“Tunatoa rai kwa vyama vya siasa kutumia jukwaa hili kuelezea ajenda zao kwa njia ya hoja badala ya matusi au uchochezi. Wananchi nao wasikilize kwa makini ilani mbalimbali ili kufanya maamuzi sahihi kwa mujibu wa maslahi ya taifa,” imesema taarifa ya Msimbe. 

Ameeleza kuwa TBN, ikiwa na wanachama zaidi ya 200 waliotapakaa kote nchini, itatumia blogu na majukwaa yake ya kidijitali kama daraja kati ya wananchi na wanasiasa, kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuelewa sera za vyama na wagombea, ili kufanya maamuzi ya msingi. 

Msimbe amesema wanablogu wote walio chini ya TBN wamepatiwa mafunzo maalum ya namna ya kuripoti kampeni kwa weledi, na hivyo wataendelea kutoa taarifa sahihi na chanya kwa lengo la kulinda uzalendo na amani ya nchi. 

“Tunaahidi kuendelea kuwa sehemu ya juhudi za Serikali katika kulinda utulivu. Tutaepuka taarifa za uchochezi na badala yake tutatumia blogu zetu kama chombo cha kudumisha amani na uzalendo,” imeeleza taarifa hiyo. 

Aidha, katika taarifa hiyo TBN imewaasa watumiaji wa mitandao ya kijamii kutanguliza maslahi ya taifa kwa kuhakikisha taarifa wanazosambaza zinajikita kwenye ukweli, uaminifu na uwajibikaji, huku ikionya dhidi ya siasa chuki, uchochezi na upotoshaji. 

“Hatutarajii kuona mitandao ya kijamii ikigeuzwa kuwa uwanja wa matusi au uchochezi. Tunawahimiza Watanzania kutumia majukwaa hayo kwa uangalifu mkubwa na kuweka mbele uzalendo wa taifa letu,” imesema taarifa hiyo. 

TBN imebainisha kuwa itaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya amani, na kwamba itasimama kidete kuhakikisha blogu zinabaki kuwa chombo cha mawasiliano chenye tija kwa taifa.

Chapisha Maoni

0 Maoni