Katika hatua ya kihistoria na kishindo
kwa sekta ya utalii nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), leo Agosti 12, 2025,
imesaini mikataba minne ya uwekezaji wa utalii kupitia utaratibu wa Uwekezaji
Mahiri (SWICA) na kampuni ya kitanzania ya Uhusiano International ICT Ltd.
Mikataba hiyo inatarajiwa kuingiza
mapato ya Dola za Marekani milioni 281.5 (sawa na Shilingi Bilioni 719 za
Kitanzania) kwa kipindi cha miaka 20 ikiwa ni wastani wa Shilingi Bilioni 36
kwa mwaka.
Hafla ya utiaji saini imefanyika
katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC),
jijini Dar es Salaam na imehusu uwekezaji katika vitalu vinne vya Burko Open
Area (Monduli – Arusha), Selous MHJ1, Selous MHJ2 na Selous ML1 (Liwale –
Lindi), vyote vikiwa chini ya kampuni ya Uhusiano International ICT Ltd
inayomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana amesema uwekezaji
huo utaimarisha sekta ya uwindaji wa kitalii na utalii wa picha, sambamba na
kuleta ajira, kuboresha huduma za jamii na kuchochea maendeleo ya wananchi
wanaoishi jirani na maeneo ya uwekezaji. Miradi ya maendeleo itakayoibuliwa na
wananchi wenyewe inakadiriwa kugharimu Dola milioni 1.8 (sawa na Shilingi
Bilioni 4.6) kwa miaka 20.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana pia
alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa juhudi zake madhubuti katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia
filamu za Amazing Tanzania na The Royal Tour, zilizochochea ongezeko la watalii
na wawekezaji.
Aliahidi kuwa Serikali itaendelea
kuboresha mazingira ya uwekezaji na kusisitiza umuhimu wa matumizi endelevu ya
rasilimali kwa kuzingatia sheria, kanuni na misingi ya uhifadhi bora. Alitoa
wito kwa wawekezaji zaidi kuja kuwekeza katika vivutio vya kipekee vya utalii
vilivyopo nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis R. Semfuko, amesema TAWA
imepiga hatua kubwa kwa kusaini mikataba minne mipya ya SWICA na kufikisha
jumla ya mikataba 13 kati ya 14 iliyopangwa
sawa na asilimia 92.3 ya lengo, hatua iliyowezesha kukusanya zaidi ya
Shilingi Bilioni 27.4 kati ya Januari 2024 na Agosti 2025.
Aidha, Meja Jenerali Semfuko
alibainisha kuwa TAWA ipo katika hatua za mwisho kusaini mkataba na kampuni ya
GBP Trading Ltd (GTL) kwa ajili ya ujenzi wa kambi za kudumu za kitalii katika
hifadhi za Kijereshi, Mpanga-Kipengere na Wami-Mbiki, hatua itakayoongeza
vitanda 240 na kupunguza uhaba wa malazi kwa watalii.
Awali, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa
TAWA, Bw. Mlage Yusuph Kabange, alisema tangu kusainiwa kwa mikataba ya awali
ya SWICA mwaka 2024, TAWA imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato kutoka Shilingi Bilioni 55 hadi Shilingi
Bilioni 87.12 katika mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia
158.2.
Aliongeza kuwa TAWA inaendelea kuweka
mazingira rafiki kwa uwekezaji, ikiwemo ujenzi wa kilomita 453.2 za barabara
kwa kiwango cha changarawe katika maeneo ya kimkakati sawa na asilimia 40 ya lengo la kujenga
kilomita 1,127 ifikapo mwaka 2026.
Kamishna Kabange alisisitiza kuwa TAWA
ipo tayari kushirikiana na wawekezaji ili kuhakikisha utekelezaji bora wa
mikataba hiyo kwa manufaa ya Taifa na wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Uhusiano
International ICT Ltd, Bw. Zahir Hassan Mulla, alitoa shukrani kwa Rais Samia
Suluhu Hassan, Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na Bodi na Menejimenti ya
TAWA kwa kuridhia pendekezo lao la uwekezaji. Alisema huu ni mwanzo mzuri kwa
wawekezaji wa ndani kuonesha uwezo wao katika sekta ya utalii.
0 Maoni