Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde
amesema Tanzania inajipanga kuwa kitovu cha utengenezaji wa bidhaa na huduma
migodini kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara kwa kuvutia uwekezaji kwenye
viwanda vya kutengeneza bidhaa za migodini na utoaji wa huduma kwenye migodi ya
ndani na nje ya nchi.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo
Jijini Dar es Salaam wakati akizindua ghala la mauzo ya vipuri vya mitambo
mikubwa na vifaa vya uchimbaji madini ambalo linamilikiwa kwa
ushirikiano kati ya Kampuni ya Shan Parts Africa ya India na Kampuni ya
ITR ya Italy.
“Nawapongeza sana Kampuni ya Shan
Parts na ITR kwa uamuzi wa kuwekeza nchini Tanzania kwenye vipuri vya mitambo
mikubwa na vifaa vya uchimbaji madini.”
Uwepo wa huduma hii hapa nchini
utapunguza uingizaji wa vipuri kutoka nje ya nchi kwa wingi na kupunguza
gharama za uendeshaji.
Sekta ya Madini ni sekta muhimu kwa
uchumi wa nchi yetu,kuwa na huduma kama hii itasaidia sana kuchochea ukuaji wa
sekta ya madini.
Tumetenga eneo la Buzwagi,Kahama kwa
ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani na huduma migodini.
Lengo ni kuhakikisha tunaifanya
Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa bidhaa na huduma migodini ya ndani ya
nchi na kwa nchi jirani zinazozunguka nchi ya Tanzania,” alisema Mavunde.
Nao Balozi wa India Nchini Mh.
Bishwadip Ney na Balozi wa Italia Mh.
Giuseppe Coppola wamepongeza ushirikiano wa kibiashara wa nchi tatu za
Tanzania,India na Italia na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na
kukuza sekta ya madini ambayo ndi sekta muhimu kwenye kuchochea ukuaji wa
uchumi wa Tanzania.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
Shan Parts Africa Ltd Ndg. Malhar Dave amesema mazingira mazuri ya uwekezaji
chini ya Uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan yamewezesha Kampuni hiyo
kuamua kuwekeza hapa Tanzania huku akibainisha Mpango wa Kampuni ni kuhakikisha
inasambaza vipuri vyenye ubora wa hali ya juu kuendana na mazingira ya
Teknolojia ya Dunia ya leo na hivyo kuchochea katika ukuaji wa sekta ya madini.
0 Maoni