Wafanyabiashara na wawekezaji wa nchini Singapore wameonesha nia ya kuongeza uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara na Tanzania kupita sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo kilimo, nishati jadidifu, viwanda vya kuongezea thamani mazao ya kilimo na uvuvi na uchumi wa kidigitali.
Wameeleza kuwa pamoja na masuala mengine wanalenga
kuimarisha biashara kati ya pande hizo mbili, kuongeza fursa za ajira kwa
vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi na sekta binafsi kwa manufaa ya wananchi
wa pande zote mbili.
Hayo yamejili kwenye Kongamano la Nane la Biashara kati ya
Afrika na Singapore (8th Africa Singapore Business Forum – ASBF) linalofanyika
jijini Singapore kuanzia tarehe 26 Agosti 2025, ambalo limewakutanisha pamoja
viongozi wa ngazi za juu serikalini, wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi za
kifedha kutoka barani Afrika na Asia.
Kongamano hilo linalohudhuriwa na washiriki zaidi ya 700
kutoka Afrika na Singapore linalenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya
kuimarisha ushirikiano wa kimkakati wa kibiashara na kiuchumi, kupitia njia
mbalimbali ikiwemo ushirikishanaji wa fursa na uzoefu wa biashara na uwekezaji,
kuibua na kuchochea miradi ya pamoja ya maendeleo.
Tanzania katika kongamono hilo imejizolea sifa, kuwa ni nchi
yenye mazingira mazuri ya uwekezaji na fursa pana za biashara kutokana na
sababu mbalimbali ikiwemo amani na usalama, sheria na sera rafiki za uwekejazi,
faida ya kijiografia inayoiwezesha kuwa kiungo katika ukanda wa Afrika
Mashariki, Kati na Kusini, jambo linaloifanya kuwa lango muhimu kwa bidhaa na
huduma kuyafikia masoko ya kikanda na kimataifa.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, akizungumza na
wafanyabiashara, wawekezaji na viongozi wa serikali kwa nyakati tofauti,
ameelezea dhamira ya Serikali ya kuendeleza mazingira rafiki kwa wawekezaji
kupitia maboresho ya sera na sheria za uwekezaji, huku ikiongozwa na dira ya
maendeleo inayozingatia misingi ya ushirikiano wa kimataifa.
Aidha kwa nayakati tofauti viongozi, wafanyabiashara na
wawekezaji wa Singapore wameelezea umuhimu wa nafasi ya Tanzania katika kukuza
biashara baina ya Afrika na Asia, huku wakionyesha shauku ya mashirika na
kampuni zao kutekeleza miradi ya pamoja na Tanzania hususan katika teknolojia
ya kilimo, huduma za kidigitali, viwanda na uchumi wa buluu.
0 Maoni