Ridhwan Kikwete asisitiza uwekezaji kwa vijana

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Ridhwan Jakaya Kikwete, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu, hususan vijana, kama msingi imara wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Makamu Spika wa Baraza la Wawakilishi la Japan, Mheshimiwa Gembá Koichiro.

Mhe. Kikwete alisema uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Japan umekuwa na faida kubwa, na sasa ni wakati wa kuimarisha zaidi ushirikiano huo kwa kulenga maendeleo ya vijana.

"Vijana wapo katikati ya ajenda yetu ya kitaifa," alisema Mhe. Kikwete, akibainisha kuwa Tanzania ina zaidi ya vijana milioni 30 wenye umri chini ya miaka 35.

Waziri Kikwete alifafanua kwamba Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, inaendelea kutekeleza programu mbalimbali zenye lengo la kuwawezesha vijana na watu wenye ulemavu.

Mipango hiyo ni pamoja na Programu ya Maendeleo ya Ujuzi ya Kitaifa, ambayo, ikiwa imefadhiliwa kupitia Kodi ya Maendeleo ya Ujuzi (SDL); na kusema kwamba imefanikiwa kuwanufaisha Watanzania 155,195 kupitia mafunzo kazini na mafunzo ya vitendo.

Vile vile, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo kwa biashara 1,126 zinazomilikiwa na wajasiriamali vijana 8,588, hivyo kukuza uchumi wa vijana.

Pia alisema katika hatua ya kurahisisha upatikanaji wa rasilimali, Serikali imetenga jumla ya ekari 274,047.33 na mita za mraba 540,642 za maeneo ya biashara kwa ajili ya vijana 193,053. Pia, serikali imeweka utaratibu wa upendeleo unaoelekeza asilimia 30 ya fursa za ununuzi wa umma kutengwa kwa ajili ya biashara zinazomilikiwa na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mhe. Kikwete pia alitoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Japan kwa msaada wake kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), ambalo limekuwa likisaidia maendeleo katika sekta mbalimbali kama kilimo, miundombinu, afya, maji, na nishati.

Alizitaja pia kampuni za Kijapani kama Konoike Construction Company Ltd., Sumitomo Mitsui Construction Company Ltd na Toyota Tsusho East Africa, akizielezea kama washirika wa maendeleo wa kutegemewa.

Mhe. Kikwete amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania ina azma ya dhati ya kuendeleza ushirikiano na Japan katika maeneo ya programu za maendeleo ya ujuzi, ujenzi wa uwezo, na uboreshaji wa rasilimali watu ili kuhakikisha vijana wanakuwa na mchango chanya katika mustakabali wa taifa.





Chapisha Maoni

0 Maoni