Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametaja mambo makuu
atakayoyapa kipaumbele ndani ya siku 100 za kwanza za awamu yake ya pili,
endapo atashinda uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika leo, Alhamisi Agosti 28, 2025, katika Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam, Dkt. Samia amesema moja ya hatua za awali ni utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, kwa kuanza na uzinduzi rasmi wa Mfumo wa Taifa wa Bima ya Afya.
Amesema kuwa mfumo huo utawalenga awali watoto, wazee na watu wenye ulemavu, huku gharama za huduma hizo zikibebwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kama hatua ya kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wote bila vikwazo vya kifedha.
“Katika siku 100 za kwanza, tutazindua mfumo huu rasmi ili kuanza kuwahudumia makundi haya yenye uhitaji mkubwa. Lengo ni kuhakikisha Watanzania wote wanafikika na huduma za afya kwa usawa,” alisema Dkt. Samia.
Aidha, mgombea huyo wa CCM ameahidi kupiga marufuku kwa hospitali yoyote nchini kuzuia ndugu kuchukua miili ya wapendwa wao pale ambapo gharama za matibabu hazijalipwa, akibainisha kuwa Serikali yake itaanzisha mfumo maalum wa kushughulikia changamoto hiyo kwa mujibu wa haki za binadamu na utu.
“Tutaanzisha utaratibu utakaowezesha familia kupata miili ya wapendwa wao bila kizuizi cha gharama, huku tukihakikisha kuwa hospitali nazo hazibebi mzigo huo kwa hasara, kwani ndugu wa marehemu watawekewa utaratimu maalum wa kulipa taratibu,” alisema.
Pamoja na mambo mengine, ameahidi serikali kugharamia
vipimo vya afya vya gharama kubwa kwa wananchi wasiokuwa na uwezo kwa maradhi
hasa yasiyoyakuambukiza na kuajiri watumishi wa afya 7,000.
Kampeni za CCM zimezinduliwa rasmi leo jijini Dar es Salaam, zikihudhuriwa na viongozi wa kitaifa wa chama hicho, wanachama, na wafuasi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Uchaguzi mkuu wa mwaka huu unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, ambapo Watanzania watawachagua Rais, wabunge na madiwani.
0 Maoni