Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC)
unaelezwa kuboresha miundombinu katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro hasa
baada ya ujenzi wa barabara na mitaro ya maji ya mvua.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya
Morogoro, Bw. Emmanuel Mkongo ambapo ameeleza kuwa miradi ya ujenzi wa mifereji
ya maji ya mvua pamoja na barabara imefikia asilimia 95 kukamilika.
"Kuna maeneo ya makazi ya watu ambapo kipindi cha mvua
yalijaa maji nakusababisha kero kwa wananchi lakini kukamilika kwa ujenzi wa
mitaro sasa maji hayatuami na kero imeondoka pia thamani ya maeneo kama viwanja
na nyumba imepanda baada ya maeneo mengi kuanza kufikika kwa urahisi",
amesema kiongozi huyo.
Aidha, Bi. Rose Munisi ambaye alikuwa mhanga wa mafuriko
kipindi cha masika ameipongeza Serikali kwa kuchukua hatua hiyo muhimu ya
ujenzi wa mifereji ya maji na kuongeza kuwa watahakikisha miundombinu hiyo
inalindwa.
"Sisi wenyewe ni walinzi wa miundombinu hii na
hatutakubali kuona mtu anatupa taka kwenye mitaro maana hapo awali tulipata
tabu kweli kipindi cha mvua," amesema Bi. Rose.
Afisa Mtendaji wa kata ya Kihonda, Bi. Tatu Khamis amesema
kuwa ujenzi wa barabara katika kata hiyo
umekuwa kiunganishi na stendi ya Treni ya Mwendokasi (SGR) na kusema kuwa licha
ya kupendezesha maeneo hayo pia barabara itakuza uchumi wa wananchi.
Kwa upande wake, Bw. Mohamed Ramadhani ambaye ni Mkazi wa Tungi amesema kuwa hapo mwanzo kabla ya ujenzi wa barabara hali ilikuwa mbaya ambapo watoto kwenda shule na hata hospitalini ilikuwa ni changamoto hasa wakati wa masika ila kwa sasa wanaweza kufanya kazi zao na kusafiri bila shida kutokana na uwepo wa barabara.
0 Maoni