Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) leo Jumatano imetangaza rasmi majina ya wagombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Akizungumza katika hafla maalum iliyofanyika katika ofisi za INEC jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, alithibitisha kuwa wagombea wote waliotimiza masharti ya kikatiba na kisheria wameteuliwa rasmi kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho kikuu cha kisiasa nchini.

Katika hatua ya kipekee mwaka huu, INEC imeanza utekelezaji wa utaratibu mpya wa kuwapatia wagombea magari mapya pamoja na dereva na mlinzi mara baada ya uteuzi wao kuthibitishwa.

Wagombea wote walikabidhiwa magari mapya aina ya Toyota Land Cruiser GXR, ambapo Kailima alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha usalama na usawa katika shughuli za kampeni.

“Utaratibu huu umewekwa kisheria. Mgombea anapokidhi vigezo vya kuteuliwa, INEC inawajibika kumkabidhi gari jipya, pamoja na dereva na mlinzi, kwa ajili ya shughuli za kampeni,” alisema Kailima.

INEC imeeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya mchakato wa uchaguzi, yanayolenga kuweka mazingira bora na salama kwa wagombea wote, bila kujali uwezo wao wa kifedha au rasilimali.