Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Charles
Kichere,ijumaa tarehe 29.08.2025 amefanya
ziara maalum kwenye jengo la Makumbusho ya Ngorongoro Lengai UNESCO
Global Geopark pamoja na kupanda mti wa kumbukumbu kwenye Eneo la Makumbusho
hayo.
CAG Kichere ambaye aliongozana na mwenyeji wake, Kamishna wa
Uhifadhi wa NCAA Bw. Abdul-Razaq Badru na menejimenti yake, amejionea na kujifunza urithi wa kitamaduni
unaoelezea upekee wa vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro, shughuli za utamaduni, urithi na
historia za makabila mbalimbali.
Akiwa ndani ya Jengo hilo, CAG Kichere alipata maelezo
kutoka kwa Afisa Uhifadhi Mkuu Dr. Agnes Gidna ambaye ni Mtaalam wa Urithi wa
Utamaduni NCAA, ambapo alionekana kufurahishwa na namna NCAA ilivyowekeza
kwenye Makumbusho hiyo ambayo itatumika kama kivutio cha utalii pamoja na
kujifunza kwa wadau mbalimbali.
Hifadhi ya jiolojia ya Ngorongoro Lengai unatokana na urithi wa kijiolojia, kiikolojia na kiutamaduni unaojumuisha Mlima Lengai wenye Volkano hai ya kipekee duniani na eneo la Ngorongoro lenye historia ya binadamu wa kale pamoja na vivutio vya utalii vilivyopo na urithi wa utamaduni wa jamii za wafugaji zilizopo ndani ya Hifadhi.
0 Maoni