Agizo la Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.
Doto Biteko alilolitoa kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa
minada yote nchini inakuwa na miundombinu itakayowawezesha Wachoma nyama, Mama
Lishe na Baba Lishe kutumia nishati Safi ya Kupikia limeanza kufanyiwa kazi
ikiwa ni utekelezaji wa ajenda ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha
wananchi wote wanatumia Nishati iliyosafi ya kupikia.
Safari hiyo ya kuhakikisha minada yote nchini inatumia
nishati safi ya kupikia, imeanzia katika Mnada wa Msalato jijini Dodoma ambapo
tarehe 21 Agosti 2025, Dkt. Biteko amegawa majiko banifu kwa Mamalishe takriban
27 wanaohudumu katika mnada huo pamoja na majiko ya kuchomea nyama.
“Kama mnavyofahamu, Mhe. Rais alitoa maelekezo kuwa
watanzania asilimia 80 ifikapo 2034 watumie nishati safi ya kupikia, maelekezo
yake yanaendelea kutekelezwa, tulianza na taasisi zinazolisha watu zaidi ya
100 kuondoa matumizi ya kuni na mkaa
ikiwemo magereza yote nchini, shule za
Sekondari , vyuo na taasisi nyinginezo lakini moja ya maeneo yaliyobaki ni
pamoja na minada ambayo inahudumia watu wengi,” amesema Dkt.Biteko.
Dkt. Biteko ameeleza kuwa kazi ya kufunga mifumo ya Nishati
Safi ya Kupikia kwenye minada ilianza na utafiti ili kupata hali halisi ya
matumizi ya nishati hiyo ambapo katika utafiti huo, asilimia 89.5 ya wachoma
nyama wote walisema hawana uelewa wowote kuhusu nishati safi ya kupikia, pia
utafiti huo umeonesha asilimia 26.3 ya wachoma nyama wamewahi kutumia nishati
safi ya kupikia na asilimia iliyobaki haijawahi kutumia. Hii ikionesha kuwa
bado kuna kazi ya kufanya kuelekea kwenye matumizi ya Nishati Safi ya kupikia.
Amesisitiza kuwa, hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali
katika Nishati Safi ya Kupikia, ni
matunda ya Mhe. Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye amejipambanua kama kama
kiongozi mwanamke anayejua machungu ya matumizi ya nishati isiyo safi na wakati
wote anaelekeza kuwa yeye anachotaka kuona
ni watu wengi hawatumii nishati isiyo safi ya kupikia.
Ameongeza kuwa, Tanzania ndiyo nchi pekee barani Afrika
ambayo imezindua Mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao
umekuwa ni mfano barani Afrika na nchi nyingine zinakuja kujifunza hivyo lazima
iwe mfano na kinara kwa kuishi yale
inayoyasema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amemuagiza Mkurugenzi wa
Jiji la Dodoma kuweka miundombinu ambayo itafanya majiko ya nishati safi ya
kupikia katika minada mkoani Dodoma kuwa
katika sehemu ya kudumu na zoezi hilo lianze mara moja.
Aidha, ameliagiza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)
kuweka kituo cha kudumu cha kuuza mkaa mbadala katika mnada wa Msalato ili
wananchi wasikwame pale wanapohitaji nishati hiyo.
Vilevile ameitaka REA, kuhakikisha majiko makubwa ya
kuchomea nyama ambayo yanatumia Nishati Safi ya Kupikia yanapatikana ili
wananchi wanaochoma nyama na wanaofuata huduma wasipoate madhara ya afya
kuanzia sasa kwenda mbele.
Dkt. Biteko ameipongeza REA na Watendaji wa Wizara ya
Nishati kwa kupoeka agizo lake kwa
haraka na kulifanyia kazi, pia amewaasa kuendelea na ubunifu utakaowawezesha
wananchi kutumia nishati safi ya kupikia na wasisahau kufanya tathmini ya
matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia katika minada hiyo.
Pia, amewaasa Mama lishe na Baba lishe kuiunga mkono ajenda
ta nishati safi ya kupikia na kuwa mabalozi wa nishati hiyo kwani watu wakiona
faida zinazotokana na kutumia nishati safi ya kupikia kutoka kwao nao watavutika kuitumia.
katika hafla hiyo,
Dkt. Biteko amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi
kubwa ya mfano katika sekta ya Nishati ambapo amesema Mkoa wa Dodoma muda si mrefu utakuwa ni kitovu cha
usambazaji umeme katika mikoa mbalimbali ikiwemo Singida, Shinyanga, Tabora,
Kigoma na Arusha na pia kitajengwa kituo kikubwa cha kusambaza umeme na
kusimamia gridi ya Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kwa upande wake
amesema walaji katika mnada wa Msalato
kwa wiki ni kati ya 2000 na 3000 hivyo kwa kutumia Nishati Safi ya
Kupikia itawezesha kuokoa mazingira kwa kuondokana na kuni na mkaa ambao
ulikuwa ukitumika kuhudumia idadi hiyo ya watu.
Aidha ameomba a kampeni hiyo ya Nishati Safi ya Kupikia
ifike kwenye masoko mbalimbali ambayo ina mama lishe na baba lishe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba
yeye amemshukuru Dkt. Biteko kwa maono yake ambayo yamewezesha Mnada wa Msalato
kufikiwa na Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni mwanzo wa kusogeza huduma kwenye
minada mingine.
Ameeleza kuwa kiwango cha matumizi ya nishati safi ya
kupikia kimepanda kutoka asilimia 6.9 ya
mwaka 2022 na hadi kufikia asilimia 20.3 na kusema kuwa kwa jinsi matumizi ya
nishatil safi ya kupikia yanavyoongezeka Serikali itatimiza lengo lake ya
kufikisha Nishati Safi ya Kupikia kwa watanzania wapatao asilimia 80 kama
alivyoagiza Mhe.Rais.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA),
Mhandisi Hassan Saidy amesema amesema katika mnada wa Msalato kuna wachoma
nyama kati ya 45 na 50 ambao watapatiwa majiko makubwa ya kuchomea nyama, pia
kuna mama lishe 27 ambao tayari wote
wamepatiwa majiko banifu.
Mwenyekiti wa Wachoma nyama katika Mnada wa Msalato, Mathias
Raphael amesema baada ya kupata elimu ya
nishati safi ya kupikia katika mnada huo
ameanza kutumia jiko linalotumia mkaa mbadala ambao amesema kuwa
unatumika kidogo huku ukichoma nyama nyingi, unakaa muda mrefu na
hauna moshi.
0 Maoni