Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, amesema ujenzi
wa maabara ya kisasa ya utafiti na uchambuzi wa madini katika mkoa wa Geita ni
hatua kubwa itakayosaidia kuwainua wachimbaji wa madini Kanda ya Ziwa na
kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini katika uchumi wa taifa.
Akizungumza leo Agosti 21, 2025 wakati wa ziara yake ya
kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara hiyo, Mhe. Mavunde amemshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali ombi la
Wizara la kujenga maabara tatu za kisasa nchini.
Amesema mbali na maabara hiyo inayojengwa Geita
itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.5, maabara nyingine itajengwa
Chunya mkoani Mbeya na maabara kubwa zaidi kimataifa itajengwa jijini Dodoma.
“Maabara hizi zitakuwa nguzo ya utafiti wa kisayansi wa
sampuli za madini, kuongeza ufanisi wa wachimbaji wadogo na kupunguza gharama
na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizi, zitakuwa na vifaa vya
kisasa zaidi,” amesema Mavunde.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti
wa Madini Tanzania (GST) ndiyo moyo wa shughuli za madini hapa nchini kupitia
kazi ya utafiti wa kijiolojia, hivyo kuanzishwa kwa kituo hicho kutasaidia
kuchochea shughuli za madini hususan katika Ukanda wa Ziwa ambao unaongoza kwa
shughuli za uchimbaji hapa nchini, zikiwemo mikoa ya kimadini ya Geita, Mbogwe,
Kagera, Mwanza, Kahama, Mara na Shinyanga.
“Kwa mwaka uliopita pekee, sekta ya madini ilikusanya
maduhuli shilingi bilioni 328 kutoka Mkoa wa Kimadini ya Geita, jambo
linaloonesha mchango mkubwa wa ukanda huu katika pato la taifa na ndiyo maana
uwekezaji huo umefanywa na Serikali hapa,” amesisitiza Mavunde.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella,
amesisitiza kuwa maabara hiyo itapunguza muda na gharama kwa wananchi waliokuwa
wakilazimika kusafiri hadi Dodoma kufuata huduma hizo.
“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa kuona umuhimu wa
kutuletea kituo hiki muhimu. Ni msaada mkubwa kwa wachimbaji na wananchi wetu
wa Kanda ya Ziwa,” amesema RC Shigella.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara wa GST, Notika
Bandeze, amesema maabara hiyo1 mpya itakuwa na vifaa na mitambo ya kisasa
zaidi, ikiwemo ya utambuzi wa madini, uchunguzi wa sampuli, pamoja na utoaji wa
taarifa za kina za kijiolojia zinazohitajika na wachimbaji na wawekezaji.
Ujenzi wa maabara ya madini Mkoani Geita unatarajiwa
kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuokoa muda na
mitaji kwa wachimbaji, na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika
maendeleo ya taifa.
0 Maoni