Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) imetoa mafunzo kwa wajumbe wa kamati za
kushughulikia malalamiko kupitia mradi wa RISE kutoka ngazi ya vijiji, kata na
wilaya katika halmashauri ya wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Akifungua mafunzo
hayo, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Handeni ambaye pia
ni Afisa Utumishi, Bi. Gladness Mwano amezitaka kamati za malalamiko kupokea na
kutafutia utatuzi malalamiko ya wananchi katika maeneo yatakayoathirika na mradi wa ujenzi wa barabara zitakazojengwa
kwa kiwango cha lami wilayani humo.
"Mradi
utakapoanza kutekelezwa katika maeneo yetu, kutakuwa na changamoto
zitakazojitokeza, sisi kama kamati ambao tunawawakilisha wananchi wengi kwenye
maeneo yetu tunatakiwa tuzingatie mafunzo ili
tuweze kupokea na kuhakikisha tunayafanyia kazi malalamiko na kuwatendea
haki wananchi kwa niaba yao," amesema.
Ameongeza kuwa
barabara zikitengenezwa wananchi watasafirisha mazao yao sokoni kama mahindi na
machungwa, wawekezaji wataongezeka na soko litakuwa na kupelekea kuongezeka kwa
uchumi wa mwananchi mmoja halmashauri na hata taifa kwa ujumla.
Naye, Meneja wa
TARURA wilaya ya Handeni, Mhandisi Judica Makyao amesema kuwa mradi wa RISE ni
wa ushirikishwaji wa wananchi lakini pia kufungua fursa za kiuchumi na mradi
unatekeleza ujenzi wa barabara ya Sindeni-Kwedikwazu (Km 38) na Michungwani -
Bondo - Kwadoya (Km 19) zote zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Naye, Mkufunzi wa
mafunzo hayo, Bi. Beatrice Mchome amesema kuwa serikali inalengo la kuleta
mradi ambao wananchi watanufaika na kufurahia ili kuhakikisha hayo taarifa
mbalimbali za utekelezaji wa mradi zimeandaliwa na elimu inaendelea kutolewa
kwa wananchi ili kupunguza malalamiko.
Wakizungumza kwenye
mafunzo hayo baadhi ya wanakamati wameipongeza serikali kwa mafunzo hayo ambapo
wameahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kujitolea ili kuwasaidia
wananchi wenzao.
0 Maoni