Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza
kuwa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikiana na Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kuhakikisha mazingira wezeshi ya biashara
na uwekezaji yanaimarishwa.
Rais Dkt. Mwinyi
amesema kuwa Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na sekta binafsi,
wajasiriamali na wawekezaji ili kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu
katika maendeleo ya Taifa.
Rais Dkt. Mwinyi
ameyasema hayo leo, tarehe 07 Julai 2025, alipofungua rasmi Maonesho ya 49 ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyofanyika katika Uwanja
wa Maonesho wa Mwalimu Julius K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais Dkt.
Mwinyi amepongeza mafanikio ya TanTrade na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa
kuendeleza maonesho hayo na kuyaweka katika viwango vya kimataifa. Amebainisha
kuwa mwaka huu, maonesho hayo yamevutia zaidi ya washiriki 5,734 kutoka ndani
na nje ya nchi, jambo linalodhihirisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha
biashara barani Afrika.
Katika hatua
nyingine, Rais Dkt. Mwinyi amezitaka Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na
TanTrade kuhakikisha kuwa elimu kuhusu Nembo Maalum ya Taifa kwa bidhaa na
huduma za Tanzania (MADE IN TANZANIA) inawafikia wazalishaji na wananchi ili
kuchochea uzalendo wa kibiashara.
Amesema uzinduzi
rasmi wa nembo hiyo unalenga kuongeza thamani na kutambulisha ubora wa bidhaa
za nchi katika soko la kimataifa.
Mapema, Rais Dkt.
Hussein Ali Mwinyi alitembelea mabanda ya maonesho ya kampuni za biashara na
huduma kutoka ndani na nje ya nchi, pamoja na kukutana na wafanyabiashara na
wajasiriamali mbalimbali.
Rais Dkt. Mwinyi
alikabidhi zawadi kwa kampuni bora yaliyofanya vizuri zaidi katika Maonesho ya
Kimataifa ya Sabasaba 2025, pamoja na Wadhamini Wakuu wa maonesho hayo.
Halikadhalika,
alipokea tuzo maalum pamoja na ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zao katika kuimarisha maonesho hayo pamoja
na kukuza mikakati ya biashara na uwekezaji nchini. Sambamba na hilo, Rais Dkt.
Mwinyi alizindua rasmi Nembo Maalum ya Taifa kwa bidhaa na huduma za Tanzania,
MADE IN TANZANIA.
0 Maoni