Waziri wa Maliasili
na Utalii, Mhe. Balozi Dkt.Pindi Chana (Mb) amesema chini ya uongozi imara wa
Rais Samia, Wizara ya Maliasili na Utalii imefanikiwa kuongeza idadi ya watalii
kufikia milioni 5.3 na mapato yatokanayo na utalii kufikia dola za kimarekani bilioni
3.9.
Ameyasema hayo katika
mkutano wa hadhara ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan alihutubia wananchi kwenye uwanja wa stendi ya zamani
Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu leo Juni 18,2025.
Mhe. Chana ameongeza
kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kutekeleza maelekezo ya Rais
Samia ya kudhibiti changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu na
kurekebisha kanuni za kifuta jasho/machozi.
"Mheshimiwa Rais
nasimama kifua mbele kusema kwamba maelekezo yako yote tumetekeleza na hapa
Bariadi tumepokea majina yasiyopungua 240 na wataalamu wako uwandani kulipa
kifuta jasho/machozi katika vijiji vya Gilya, Senta, Nyamikoma,
Salalia,Mwasilimbi,Matongo, Ng’alita, Mwandama,Mwantimba, Ihusi, Igabanyiro,
Masewa na Mauchumu " amesema Mhe. Chana.
Sambamba na hilo Mhe.
Chana amefafanua kuwa Serikali imeendelea kujenga vituo vya askari kudhibiti
wanyamapori wakali na waharibifu na kwa Bariadi vimejengwa katika maeneo ya
Handajega, Duma na Ndabaka na vinaendelea kuongezwa.
Aidha amesema
Serikali inatoa elimu ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa vijana
(Village Game Scouts) kupitia chuo cha
Likuyu Sekamaganga kilicho chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
"Tumetoa mafunzo
kwa askari wa vijiji (VGS) wasiopungua 390 kutoka vijiji takribani 13 vya
Nyamikoma, Senta, Igabanilo, Mwatimba, Matongo, Salaliya, Mwauchumu, Chungu
,Damidami, Halawa, Ihusi, Mwasilimbi na Mwasinasi.
Mhe. Chana amesema
Wizara inaendelea kufunga kola tembo viongozi ili kuweza kufuatilia mienendo
yao, kuweka minara (observation tower) na kugawa vifaa mbalimbali vya kudhibiti
tembo ikiwemo tochi, vuvuzela,filimbi, ndegenyuki na kugawa mabomu baridi
katika vijiji mbalimbali ikiwemo Nyamikoma, Senta,Igabanilo, Mwantimba,
Matongo,Salalia, Mwauchumu, CChungu,Damidami, Halawa, Ihusi, Mwasilimbi na
Mwasinasi.
Katika hatua
nyingine, Mhe. Chana amemshukuru Rais Samia kwa kuridhia mapato ya retention ya
asilimia 51 kubaki kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa ajili ya kuendeleza uhifadhi na utalii.
0 Maoni