Imeelezwa kwamba
uwepo wa mvua nyingi jijijini Dar es Salaam umepelekea ujenzi wa barabara
katika maeneo yenye zabuni kusimama kufanya kazi katika kipindi cha miezi
miwili.
Hayo yameelezwa na
Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Dar es
Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga wakati akikagua maeneo ambayo yapo chini ya
wazabuni.
Mhandisi Mkinga amekagua barabara ya
Tabata-Mazda (mita 500), Tabata-Kinyerezi kuelekea Sokoni (kiwango cha zege)
pamoja na barabara ya Kivule-Msongola (km 9) na barabara kuelekea hospitali ya
wilaya na Majohe (Km. 2.7).
“Kama tulivyotoa
taarifa mwanzo kwamba kazi nyingi zilikuwa zimesimama kutokana na uwepo wa mvua
nyingi zilizonyesha hivyo kwasasa tumeshawaagiza wakandarasi warudi ‘site’ na
kuanza kazi mara moja”.
“Wakati wa mvua
nyingi wakandarasi hawakuweza kukusanya malighafi na hata kuingia kwenye
machimbo, pia huwezi kuweka ‘material’ ya udongo kipindi hicho” aliongeza Mhandisi Mkinga kusema.
Hata hivyo, Mhandisi Mkinga aliwataka wakandarasi wote waliopewa zabuni za ujenzi wa barabara katika
mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha wanaingia kazini ili kazi walizopewa
zikamilike kwa wakati.
Kwa barabara ya
Msongola-Kivule, Mhandisi Mkinga amemuagiza Mkandarasi kuendelea na kazi hiyo
hadi Desemba mwaka huu awe ameshatoka hatua za awali na kubakiza kuweka tabata
la lami pamoja na mifereji.
“Kama unavyoona
kuelekea hospitali ya wilaya na Majohe, ilikuwa barabara mbovu na wananchi
wamekuwa wakilalamikia ila kwa sasa hamna kazi iliyosimama na maendeleo ya
mradi ni mazuri.”
Naye, Meneja wa Ilala
Mhandisi John Magori amesema wataendelea kuwabana wakandarasi kuhakikisha
maeneo yote yenye mikataba yanafanyiwa kazi kwa wakati ili kusudi changamoto za
barabara ziishe.
Amesema, wakandarasi
katika kata zote wameshaanza kurudi ‘site’ na kazi zimeanza ikiwemo katikati ya
jiji, Tabata, Kitunda na Upanga.
Mkazi wa Msongola,
Bw. Peter Marwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa ujenzi wa barabara hizo kwani itawaondolea adha ya usafiri
katika Kata ya Msongola-Jimbo la Kivule.
Wakati huo huo, Mkandarasi anayejenga barabara ya Segerea,
Mhandisi Lookman Msanguka amesema kazi zilisimama kwa kipindi fulani ila kwa
sasa kazi zinaendelea na hivyo ameaahidi kufanya kazi na kukamilisha mradi huo kama
ulivyopangwa.
“Changamoto
zilikuwepo kutokana na mvua kwani huwezi
kufanya kazi ya zege na kushindilia vifusi kipindi cha mvua hivyo tulisimama
kwa miezi miwili ila kwasasa tunapambana ili kwenda sawa na kilichokuwepo
kwenye mikataba.”
0 Maoni