Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Juni 23, 2025 alifanya ziara katika
bustani ya wanyamapori ya Tabora, maarufu kama Tabora ZOO, kwa lengo la kukagua
na kuona usimamizi wa bustani hiyo ambapo alitumia fursa hiyo kuwahamasisha
Watanzania hususani wa ukanda wa magharibi, wakazi wa Mkoa wa Tabora na Mikoa
ya jirani kutembelea kivutio hicho cha kipekee ambacho kipo Katikati ya Mkoa wa
Tabora.
Katika ziara hiyo,
Dkt. Abbasi ameonesha kuridhishwa na uwepo wa bustani hiyo ambayo ni hazina ya
vivutio vya wanyamapori na mazingira asilia. Ameeleza kuwa Tabora ZOO ni sehemu
muhimu ya utalii wa ndani ambayo Serikali imejipanga kuhakikisha inafanya
maboresho makubwa ya miundombinu ili kuvutia watalii wengi zaidi.
"Hii ni Hifadhi
ya kipekee, kuwa na eneo la heka zaidi ya 27 Katikati ya Manispaa ya Tabora au
mji ni jambo kubwa, kwahiyo niwaombe wakazi wa Tabora, hii ni Johari yenu, ni
bustani iliyowekwa Kwa ajili yenu mje kupumzika, kujifunza lakini si tu wakazi
wa Tabora bali pia wanafunzi wa vyuo mbalimbali na watu wa ukanda huu
tunawakaribisha sana," alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, Katibu Mkuu
huyo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha bustani hiyo kwa kuongeza
miundombinu ikiwemo sehemu za
watalii kupumzika na burudani kama
michezo ya watoto, maeneo ya chakula,
vinywaji pamoja na kuongeza Idadi ya wanyamapori na mabwawa ya maji ili kuongeza mvuto zaidi kwa watalii.
Katika ziara hiyo
Dkt. Abbasi aliweza kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kupitia bustani hiyo ya wanyamapori na
maendelezo yaliyofanyika ikiwemo ujenzi wa kituo cha maelezo Kwa wageni (VIC,),
mabanda ya wanyamapori, ongezeko la wanyamapori wakiwemo simba, chui, duma,
fisi na wengine wa aina mbalimbali.
Tabora ZOO ambayo ni
mojawapo ya bustani chache za wanyamapori
nchini zilizopo katika maeneo ya miji imeendelea kuwa kivutio cha kipekee Kwa watalii kutokana
na mandhari nzuri na mazingira tulivu
ambavyo vinaiweka bustani hii katika nafasi ya juu Kwa utalii wa mijini (Urban
Wildlife Tourism).
0 Maoni