Juni 28 mwaka huu Tanzania itaweka rekodi nyingine muhimu katika sekta ya utalii kwa kuwa mwenyeji wa Tuzo za 32 za Utalii Duniani Kanda ya Afrika (World Tourism Awards Africa and Indian Ocean Gala Ceremony 2025) zitakazofanyika Rotana Hotel jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana Juni
18, 2025, baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii na mabanda
mengine kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini
Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, amesema uenyeji wa
Tanzania katika tuzo hizo ni matokeo ya heshima kubwa ambayo nchi yetu inayo
duniani katika utalii kutokana na kazi kubwa ya Rais wa Awamu ya Sita Dkt.
Samia Suluhu Hassan.
“Sisi ndio nchi
inayoshikilia Tuzo ya Kuwa Kivutio Bora Duniani na Afrika kwa utalii wa safari
kwa mwaka 2024; kuletwa Tuzo hizo hapa nchini ni matokeo ya kazi kubwa ambayo
Rais amefanya kuitangaza nchi yetu kupitia Royal Tour na juhudi nyingine,”
amesema Dkt. Abbasi na kuongeza:
“Tayari maandalizi
yanakamilika kupitia Bodi yetu ya Utalii na tunatarajia tukio hilo
litakaloitangaza Tanzania duniani kuhudhuriwa na wadau wa utalii takribani 500
kutoka mataifa mbalimbali Afrika na duniani na mamilioni kufuatilia kupitia
televisheni na mitandao ya kijamii.”
0 Maoni