WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuiimarisha Taasisi ya Elimu Tanzania
(TET) ili ifikie maono ya kuwa kitovu maridhawa cha ubora katika uandaaji,
ukuzaji na ubunifu wa mitaala.
Amesema kuwa TET ni
moyo wa ukuaji wa elimu nchini na hasa kwa kuwa ndiyo inayojenga msingi wa
elimu kuanzia Darasa la Awali mpaka Kidato cha Sita.
Amesema hayo leo
Jumanne (Juni 17, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania
(TET) yanayofanyika katika viwanja vya Taasisi hiyo, Bamaga Jijini Dar es
Salaam.
“Serikali inatambua
wakuza mitaala wanafanya kazi kwa bidii, weledi, maarifa na moyo wa kizalendo
sana. Hivyo, niwahakikishia Watanzania wote kuwa, wakati wote Serikali,
itaendelea kuimarisha utendaji wa TET ili kwenda sambamba na kazi ya ukuaji wa
sayansi na teknolojia.”
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
iimarishe ushirikiano na taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi ili TET ipate
uzoefu zaidi katika kuandaa mitaala, kuandaa vifaa vya mtaala na kutoa mafunzo
endelevu ya walimu kazini.
“Hii inamaana ya
kuwepo kwa ziara za ndani na nje ya nchi kwenda kupata uzoefu, msijifungie hapa
tu, nendeni mkaone wenzenu wanafanya nini, ili muendelee kufanya maboresho
zaidi kwenye taasisi yenu.”
mmeeleza mafanikio
kadhaa yaliyopatikana katika masuala ya uandaaji wa mitaala, vitabu vya kiada
na vifaa vingine vya utekelezaji wa mitaala, matumizi ya TEHAMA na teknolojia
nyingine katika utoaji wa huduma zenu pamoja na utoaji wa mafunzo kwa walimu na
wasimamizi wa utekelezaji wa mitaala.
Aidha, Mheshimiwa
Majaliwa ameipongeza taasisi hiyo kwa mapinduzi makubwa ya matumizi ya TEHAMA
na mifumo wa kidijitali. “Katika hili nimejionea mwenyewe katika maonesho yenu
kuwa hata walimu wenye mahitaji maalumu wanaweza kutumia maktaba mtandao na
mfumo wa kidijitali haya ni mapinduzi makubwa katika kipindi hiki cha miaka 50.”
Kwa Upande wake,
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amempongeza Rais
Dkt. Samia kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya elimu nchini “Ni
kazi kubwa sana imefanyika katika kuandaa mitaala mipya, wakati Serikali
ilipokuwa inazindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023
tulikuwa tunatekeleza maono yake.”
Naye, Mkurugenzi Mkuu
wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba amesema kuwa katika kipindi cha
miaka 50, Serikali kupitia TET imefanikiwa kuongeza hazina ya vitabu vya ziada,
rejea, Riwaya, Hadithi, ushairi na aina nyingine ya uandishi bunifu pamoja na
moduli na maudhui ya kielektroniki yanayolenga kuwaongezea maarifa wanafunzi
kwa kutathmini vitabu vya ziada aina 1446 vinavyoandikwa na
wachapishaji binafsi.



0 Maoni