Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa amezindua mitambo kumi ya uchorongaji na vifaa vya utafiti wa madini
yenye thamani wa shilingi bilioni 12.41 kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambayo
itapunguza changamoto za wachimbaji wadogo ya kufanya uchimbaji bila kuwa na
taarifa za kijiolojia.
Akizungumza baada ya
uzinduzi huo uliofanyika leo Jumanne (Juni 24, 2025) kwenye Kituo cha Mikutano
cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa hatua hiyo
ni mwendelezo wa juhudi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha shughuli za
wachimbaji wadogo wa madini na kuwawezesha kuongeza uzalishaji.
“Oktoba 2023 Rais
Dkt. Samia, alizindua mitambo mitano ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji
wadogo. Kutokana na wingi wa wachimbaji wadogo nchini na mwitikio chanya wa
wachimbaji wadogo alielekeza Wizara ya Madini kuongeza mitambo mingine.”
“Mitambo hiyo mitano
imeshatoa huduma ya uchorongaji kwa wachimbaji 16 katika maeneo mbalimbali
nchini na kuchoronga jumla ya mita 3,450.37.”
Kadhalika Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa kuongezeka kwa mitambo ya uchorongaji maalumu kwa
wachimbaji wadogo kutaleta mageuzi na manufaa makubwa katika sekta madini.
“Moja ya faida kubwa za mitambo hiyo, ni pamoja na kuongeza chachu ya ukuaji wa
shughuli za wachimbaji wadogo nchini kwa kuwa itawawezesha upatikanaji wa
taarifa za uhakika za jiolojia.”
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wachimbaji wadogo kuendelea kuuza
madini katika viwanda vya ndani vya kusafisha dhahabu ili kuendelea kuchochea
ukuaji wa uchumi nchini. “Na wale ambao wanashughulika na usafishaji wa madini,
nendeni mkauze kwenye masoko yetu 43 yaliyopo na vile vituo 109, hakikisheni
mzunguko wa madini unaanza kunufaisha Taifa letu badala ya kutorosha madini,
kama kweli wewe ni mzalendo wa Taifa hili, popote utakapozalisha madini nenda
kwenye masoko ya ndani ya nchi.”
Waziri wa Madini
Anthony Mavunde amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha unaoishia, Sekta ya
Madini imefanikiwa kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali kiasi cha shilingi
trilioni 1.01. “Pamoja na maboresho haya, kwasasa katika benki Kuu ya Tanzania
inahifadhi ya tani 5.7 na kuifanya Tanzania kuwa ndani ya kumi bora ya nchi
zenye hifadhi ya dhahabu Afrika”.
Aidha, ameongeza kuwa
katika miaka miaka ya minne ya Rais Dkt. Samia madarakani, sekta ya madini
imeshuhudiwa ikifanya mapinduzi makubwa ikiwemo kuongeza mchango wake katika
pato la taifa ambapo mpaka sasa inachangia asilimia 10.1 kabla ya mwaka wa
kimalengo kufika.
Naye, Rais wa
Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina
ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa
uamuzi wake wa kuamua kuisimamia sekta ya madini ikiwemo kuwawezesha wachimbaji
wadogo nchini.
“Madini ni sayansi na
madini ni biashara, kwa maboresho haya, sasa watanzania wanachagamkia fursa
katika sekta ya madini, wachimbaji sasa wanatosha kuchimba, wachimbaji wadogo
tupo pamoja na Serikali yetu, hakika imetuheshimisha.”
0 Maoni