Imeelezwa kuwa kiwanda cha Mineral Access Systems Tanzania Ltd (MAST), ambacho ni cha Kwanza nchini kwa Kuchenjua Madini ya Shaba kwa Teknolojia ya Kisasa, kimeiweka Chunya kwenye ramani ya dunia kama mzalishaji wa madini hayo kufuatia kuanzishwa kwa kiwanda hicho na kwamba, uwepo wake ni matumaini makubwa kwa wananchi na taifa.
Hayo yamebainishwa jana Juni 18, 2025, na
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na niaba
ya Mhe. Dkt. Samia Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya
kuweka jiwe la msingi na kuzindua kiwanda hicho kilichopo katika Kata ya
Mbugani, Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya.
Amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ni uthibitisho wa vitendo na
dhamira ya Serikali ya kuongeza thamani madini hapa nchini, na kwamba uwekezaji
huo mkubwa kutoka kwa kampuni ya MAST ni ushahidi wa kuimarika kwa mazingira ya
biashara na uwekezaji nchini.
Aidha, Mhe. Majaliwa amefafanua kuwa kiwanda hicho kinaendana
kikamilifu na matakwa ya Sera ya Madini, kwa kuleta mapinduzi katika
kuhamasisha uongezaji thamani ndani ya nchi, kuhamasisha matumizi ya teknolojia
ya kisasa, pamoja na kuhifadhi mazingira katika maeneo ya shughuli za madini.
"Hii ni hatua ya
msingi katika kuifanya Tanzania isiwe tu nchi ya kuchimba madini bali pia kuwa
nchi ya viwanda vya kuongeza thamani ya madini na kutengeneza bidhaa zenye
thamani kubwa zinazotokana na madini," amesisitiza Mhe. Majaliwa.
✅ Ajenda
za Msisitizo wa Serikali kwa Sekta ya Madini:
Waziri Mkuu amesema
kuwa msisitizo mkubwa umewekwa katika kuhakikisha kuwa madini yote
yanayochimbwa nchini yanaongezewa thamani ndani ya nchi na kuwa hatua hiyo
inalenga kuongeza ajira, mapato ya serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali, na
kuendeleza viwanda vya ndani vinavyotegemea malighafi ya madini, hivyo
kulifanya taifa kuwa na uchumi shindani kimataifa.
Aidha, ameelekeza
kuwa shughuli zote za uchimbaji wa madini zitekelezwe kwa kuzingatia utunzaji
wa mazingira. Hii inajumuisha matumizi ya teknolojia rafiki, urejeshaji wa
maeneo baada ya uchimbaji, na kuzuia uchafuzi wa mazingira ili kulinda maisha
ya watu, vyanzo vya maji na viumbe hai.
Katika kulinda
maslahi ya jamii zinazozunguka migodi, Mhe. Majaliwa amesisitiza kuwa
wawekezaji waajiri wakazi wa maeneo hayo kwa nafasi zisizohitaji ujuzi maalum. Hii
itasaidia kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza kipato kwa wananchi wa maeneo
ya miradi.
Vilevile, Waziri Mkuu
amesema kuwa wawekezaji wote wanapaswa kulipa tozo na ushuru wa serikali
ikiwemo mrabaha. Utii wa masharti haya ni muhimu kwa Serikali kupata mapato ya
kugharamia huduma za kijamii kama elimu, afya, na miundombinu.
Ameagiza pia kuwa
kampuni zote zitekeleze wajibu wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa kuhakikisha
jamii zinazozunguka maeneo ya miradi zinanufaika na huduma kama vile shule,
barabara, zahanati au maji safi.
✅ Kauli
ya Mkurugenzi wa MAST
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa MAST, Bw. Godfrey Kente, amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa
kiwanda hicho ni kuchenjua mashapo ya madini ya shaba yenye kiwango cha chini
(0.5% - 2%) kutoka eneo la Mbugani, Chunya, na kuyapandisha thamani hadi
kufikia kiwango cha asilimia 75 ya shaba kupitia teknolojia ya leaching na
cementation.
Ameeleza kuwa kwa
sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata tani 31,200 za mashapo ya shaba kwa
mwezi, ambapo tani 27,200 zinatoka kwenye mgodi wa kampuni hiyo na tani 4,000
zitanunuliwa kutoka kwa wachimbaji wadogo nchini.
✅ Mpango
wa Ujenzi wa Viwanda Nyingine
Kente ameeleza kuwa
MAST inatarajia kujenga viwanda vingine vitatu vya kuchenjua madini ya shaba
katika mikoa ya Manyara–Simanjiro, Ruvuma–Mbesa (Tunduru), na Dodoma, ambapo
kila kiwanda kitapata wafanyakazi zaidi ya 500 na kuchangia kwa athari za
kiuchumi zenye thamani ya zaidi ya USD milioni 40 kwa mwaka.
"Mhe. Waziri
Mkuu, tayari kiwanda hiki kimetoa ajira kwa wafanyakazi 254, wakiwemo 209
waliopo moja kwa moja chini ya MAST na 45 kupitia wakandarasi. Kati yao,
Watanzania 205 wamenufaika moja kwa moja, ambapo takribani 60% wanatoka Mkoa wa
Mbeya, hususan Wilaya ya Chunya," amesema Kente.
Ameongeza kuwa MAST
ni kampuni ya Kitanzania iliyoanzishwa mwaka 2011, ikiwa na dhamira ya
kuendeleza biashara ya madini kwa njia jumuishi na endelevu, na kwamba imekuwa
ikishiriki katika biashara ya madini ya kimkakati kama shaba, nikeli na
manganese ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo.
✅ Maelezo
ya Naibu Waziri wa Madini
Awali, akimkaribisha
Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, amesema kuwa Ilani ya
CCM ya 2020 – 2025 imeelekeza ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini
nchini, kama mkakati wa kuifanya Tanzania isiwe mzalishaji tu wa malighafi bali
pia mzalishaji wa bidhaa zenye thamani kubwa.
Aidha, Dkt. Kiruswa
ameeleza kuwa kiwanda cha MAST ni miongoni mwa viwanda tisa (9) vinavyotarajiwa
kujengwa nchini kwa ajili ya kuongeza thamani ya madini muhimu. Juhudi hizi ni
sehemu ya mpango wa taifa wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji wa
madini barani Afrika, na kuongeza uwezo wa kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani
badala ya malighafi.
0 Maoni