Bodi ya Wakurugenzi
na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)
inayoongozwa na Mej. Jen (Mstaafu) Hamis Semfuko imefanya ziara ya kikazi
katika Visiwa vya Zanzibar kwa lengo la kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji
katika masuala ya utalii ikiwemo uwekezaji wa Bustani ya Wanyamapori Zanzibar
katika Hifadhi ya Jambiani Muyuni.
Akizungumza baada ya
ziara hiyo iliyofanyika Juni 25, 2025, Mej. Jen (Mstaafu) Semfuko alisema TAWA
iliona fursa ya uwekezaji wa Bustani ya Wanyamapori Zanzibar baada ya kuona
mwitikio mkubwa wa wananchi wa kuangalia wanyamapori katika Tamasha la
Kizimkazi.
“TAWA imekua ikileta
wanyamapori katika Tamasha la Kizimkazi kwa miaka miwili na katika tamasha hilo
matamanio makubwa ya wananchi ilikuwa ni kuona wanyamapori,” alisema Semfuko.
Semfuko amesema
uwekezaji wa Bustani ya Wanyamapori Zanzibar unatarajiwa kuwa wa kisasa na
ukikamilika utakuwa na faida nyingi zikiwemo kuongeza vivutio vya utalii, kuongezeka kwa ajira kwa wananchi wanaoishi
pembezoni mwa hifadhi pamoja na kuongezeka kwa mapato ya Serikali kwa ujumla.
Naye, Habibu
Al-Majid, Mkuu wa Hifadhi ya Jambiani Muyuni aliishukuru TAWA kwa kuona fursa
ya uwekezaji katika hifadhi hiyo na alisema kuwa uwekezaji huo wa Bustani ya
wanyamapori utaenda kuchochea utalii katika Mkoa wa Kusini.
“Uwepo wa TAWA kwa
kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika hifadhi ya Jambiani
Muyuni utaleta chachu kubwa ya maendeleo ya utalii na kukuza kipato cha Taifa
na jamii kwa ujumla,” alisema Al-Majid.
Aidha, Habibu
aliongeza kwa kusema kuwa eneo hili ni miongoni mwa vivutio muhimu
vinavyopatikana katika Mkoa wa Kusini na imesheheni bioanui tofauti tofauti
zikiwemo spishi mbalimbali za wanyamapori kama vile kimapunju na spishi za
ndege kama vile jogoo mwitu.
Awali, Bodi ya
Wakurugenzi ilikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja,
Mhe. Ayoub Mohammed Mahamoud kuhusu uwekezaji unaotarajiwa wa Bustani ya
Wanyamapori katika Mkoa wake.




0 Maoni