Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof.
Palamagamba Kabudi, ameitambulisha rasmi Bungeni Bodi ya Ithibati ya Waandishi
wa Habari (JAB) na kubainisha kwamba katika kutekeleza majukumu yake kwa Mwaka
wa Fedha 2025/26 itaanza kwa kutoa mafunzo kupitia Mfuko wa Mafunzo kwa
Waandishi wa Habari.
Waziri Kabudi ametoa utambulisho huo leo tarehe 07 Mei, 2025
Bungeni Mjini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha
2025/2026.
“Sheria ya Huduma za Habari Sura 229 kwa sasa inaelekeza
uundwaji wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari. Napenda kulifahamisha
Bunge lako tukufu kuwa tayari Bodi hiyo imeishaundwa na ilizinduliwa rasmi
tarehe 3 Machi, 2025 na kuanza kufanya kazi. Bodi hii inaongozwa na Mwandishi
wa Habari mahiri na mkongwe kwenye tasnia ya habari, Bw. Tido Mhando,” amesema
Waziri Kabudi.
Waziri Kabudi amesema mbali na majukumu ya msingi ya Bodi ya
Ithibati ya Waandishi wa Habari ambayo ni kusimamia maadili ya waandishi wa
habari na weledi wa kitaaluma katika kuandika habari pia itausimamia Mfuko wa
Mafunzo kwa Waandishi wa Habari.
“Mfuko wa Mafunzo kwa Waandishi wa Habari unalenga kuwezesha
mafunzo kwa waandishi wa habari, kusaidia uzalishaji maudhui ya ndani na pia
kuwezesha tafiti katika masuala ya uandishi wa habari na mawasiliano kwa umma,”
amesema Waziri Kabudi.
Amesema ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu hayo yote
ikiwemo uzalishaji wa maudhui ya ndani, Mfuko huo chini ya Bodi utaanza
kusaidia waandishi wa habari kuwa na vifaa vya kisasa ili kuwawezesha kushiriki
kikamilifu katika kutengeneza maudhui ya ndani.
Waziri Kabudi amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara hiyo itaendelea na majukumu yake ya usimamizi wa Sekta ya Habari ili kuhakikisha inaendelea kukua na kuwa na mchango mkubwa kwa Taifa na kuhakikisha Watanzania wanapata taarifa sahihi na zilizochakatwa kwa weledi wa hali ya juu na waandishi wa habari wenye sifa.
Na. Mwandishi Wetu - JAB


0 Maoni