Waziri wa Kilimo wa
Japan Taku Eto amejikuta akilazimika kujiuzulu wadhifa wake baada ya kuongelea
kwa mzaha tatizo la kupanda kwa bei ya mchele nchini humo.
Waziri huyo alipotangaza kuwa hajawahi kununua mchele
kwa sababu wafuasi wake humpa "wa kutosha" kama zawadi, alitarajia kuchekesha
tu. Lakini mdomo ulikiponza kichwa.
Japan inakumbwa na
mgogoro wa gharama ya maisha kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa, na hili
limeathiri chakula pendwa sana cha mchele.
Bei ya mchele
imepanda maradufu Japan katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, na aina
zinazoagizwa kutoka nje ni chache sana.
Eto ameomba radhi,
akisema kuwa alipinduka mipaka kwa kauli yake aliyotoa Jumapili katika shughuli
ya kuchangisha fedha huko nyumbani kwao.
Waziri Eto alijiuzulu
baada ya vyama vya upinzani kutishia kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani
naye.
Kuondoka kwake
kunaleta pigo jipya kwa serikali ya wachache inayoongozwa na Waziri Mkuu
Shigeru Ishiba, ambayo tayari ilikuwa inakumbwa na kuporomoka kwa uungwaji
mkono wa umma.
0 Maoni