Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina
(OMH), imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato yasiyo
ya kodi, baada ya kukusanya Sh749 bilioni hadi kufikia Mei 7, 2025 , sawa na
asilimia 67 ya lengo la mwaka wa fedha 2024/25 la Sh1.113 trilioni.
Taarifa hiyo ilitolewa Jumatano, May 7, 2025 na Bi.
Lightness Mauki, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya
mashirika ya kibiashara kutoka OMH.
Bi. Mauki alikuwa anazungumza kuelekea Siku ya Gawio ‘Gawio
Day’ itakayoadhimishwa Juni 6, 2025, Ikulu ya Chamwino, Dodoma, ambapo Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kupokea
gawio kutoka taasisi mbalimbali za umma.
Akizungumza hapo awali, Jumanne usiku, katika kipindi
maalumu cha dakika 30 cha TBC, Bi. Mauki alisema taasisi nyingi bado
zinaendelea na mikutano yao ya wanahisa (AGMs), hivyo OMH ina uhakika wa
kufikia lengo la mwaka.
Maudhui ya kipindi hicho cha TBC yalilenga kuonesha mchango
wa mashirika na taasisi za umma katika maendeleo ya Taifa.
“Ni imani yetu tutampatia gawio nono Mheshimiwa Rais mwezi
Juni 6,” alisema kwa kujiamini.
Takwimu zinaonesha kuwa kati ya Sh749 bilioni zilizokusanywa
hadi Mei 7, gawio kutoka kwa mashirika ya umma na Kampuni ambazo serikali ina
umiliki wa hisa chache limechangia asilimia 63 ya mapato hayo, huku mchango wa
asilimia 15 ya mapato ghafi unaokwenda moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa
Serikali ukichangia asilimia 29.
Mapato mengineyo, yakiwemo Marejesho ya mikopo na riba
(onlending), na Mawasilisho yatokanayo na mtambo wa TTMS, yamechangia asilimia
8 ya jumla hiyo.
Kiasi ambacho kimekusanywa hadi kufikia Mei 7 mwaka huu ni
kikubwa ukilinganisha na mwaka uliopita kipindi kama hiki, ambapo makusanyo
yalikuwa Sh500 bilioni — ikiwa ni ongezeko la asilimia 50.
Siri ya mafanikio
Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu amesema kuwa
mafanikio ya OMH yanatokana na utekelezaji wa mikakati ya usimamizi iliyowekwa
na ofisi hiyo.
Alisema ofisi yake imekuwa ikifanya mapaitio ya mikataba ya
wanahisa, mikataba ya uendeshaji pamoja na mikataba ya kiufundi ili kupunguza
gharama za uendeshaji na kuongeza gawio la Serikali.
Aliongeza kuwa matumizi ya mifumo ya TEHAMA, hasa mfumo wa
Serikali wa kukusanya mapato kielektroniki (GePG), yameongeza uwazi, weledi na
kasi ya ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza Alhamis Asubuhi wakati wa kipindi maalumu cha
Kumepambazuka cha Redio One, Bi. Neema Musomba, Mkurugenzi wa Huduma za
Kimenejimenti kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, alisema uchambuzi wa taarifa za utendaji wa taasisi
kila robo mwaka, nusu mwaka na mwisho wa mwaka, pamoja na uhakiki wa bajeti
kabla ya kuidhinishwa, umewezesha serikali kuwa na udhibiti wa karibu zaidi wa
mwenendo wa kifedha wa mashirika hayo.
Kwa upande mwingine, alibainisha kuwa tathmini za usimamizi
wa utekelezaji wa mikataba kati ya Msajili wa Hazina na Wenyeviti wa Bodi za
mashirika zimeimarika, jambo lililoleta uwajibikaji wa moja kwa moja kwa
viongozi wa taasisi hizo.
Mapato yasiyo ya kodi: Nguzo ya maendeleo ya Taifa
Mapato yasiyo ya kodi yameendelea kuwa mhimili wa kugharamia
huduma za msingi kama elimu, afya, maji safi na miundombinu.
Kupitia makusanyo haya, serikali imepunguza utegemezi wake
kwa misaada ya wahisani na mikopo kutoka nje ya nchi, hali inayochochea uhuru
wa kiuchumi na sera.
"Mapato hayo huchochea uwajibikaji wa mashirika ya
umma, huongeza ufanisi wa utendaji kazi, na hujenga imani ya wananchi kwa
taasisi za umma," alisema Bi. Musomba.
“Gawio si tu fedha – ni ishara ya utendaji bora,
uwajibikaji, na ushiriki wa taasisi katika maendeleo ya Taifa."
OMH imeelekeza taasisi zote ambazo bado hazijawasilisha gawio la mwaka huu kuhakikisha zimefanya hivyo kabla ya tarehe 30 Juni, 2025, ili kusaidia kufanikisha mipango ya serikali kwa mwaka wa fedha unaoendelea.
0 Maoni