MKOA wa Lindi
unatarajiwa kuwa lango kuu la uchimbaji wa madini kutokana na kuonekana kuwa na
aina zaidi ya 10 za madini mbalimbali yanayopatikana kwa wingi ikiwemo madini ya
kimkakati kama Kinywe (Graphite) na Nickel.
Akizungumza katika
mahojiano maalum, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emmanuel Shija
amesema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania
(GST) mwaka 2024 kwa kutumia ndege nyuki umebaini uwepo wa kiasi kikubwa cha
madini mkakati ya Kinywe katika eneo la Ruangwa katika Mkoa wa Lindi.
Aina nyingine ya
madini yanayotambuliwa kuwepo ni pamoja na madini yenye asili ya Chuma, kama Nickel, Dhahabu,
Shaba, Manganese na Madini ya viwandani
ambayo ni Jasi, Chokaa, Chuma na Chumvi.
Mhandisi Shija
amesema pia Mkoa wa Lindi unazalisha kwa wingi madini ya viwandani ya Gypsum
ambayo yanatumika zaidi kwenye viwanda vya saruji na 'gypsum board' vilivyopo
ndani ya nchi na nchi jirani.
“Mkoa wa Lindi kwa sasa tunautambulisha kama ‘The
Future Mineral Hub of Tanzania' (kitovu cha uchimbaji madini Tanzania), pamoja na kutokuwa na miradi mingi mikubwa
kwa sasa ni mategemeo yetu kuwa ndani ya
miaka michache ijayo tunategemea kuwa na miradi mikubwa ya madini ndani ya mkoa
wetu," amesema Mhandisi Shija na kuongeza.
"Hii ni kutokana
na ukweli kuwa kuna upatikanaji wa
madini mbalimbali kwa kiwango kikubwa," amesema.
Amesema, kwa sasa upo mradi wa uchimbaji wa kati wa
Lindi Jumbo ambao umeanza kuzalisha madini ya kinywe yenye ubora wa hali ya juu
kwa ajili ya matumizi ya betri na vifaa vya kielektroniki.
“Hali ya uzalishaji
ni nzuri kwenye makusanyo tuna aina kuu tatu za madini zenye mchango mkubwa,
ambazo ni Nickel yanaongoza kwa
kuchangia asilimia 35 ya makusanyo,
lakini pia tuna madini ya Dhahabu yanayochangia
asilimia 30 yakifuatiwa na madini ya Gypsum yenye mchango wa asilimia
20," amesema Shija.
Aidha, Mhandisi Shija
amesema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 walipangiwa kukusanya jumla ya
Shilingi za kitanzania Bilioni 7.5 na wamekamilisha lengo la makusanyo ya
maduhuli hayo tangu Mei 5 mwaka huu.
“Mpaka sasa
tumeshakusanya shilingi Bilioni 7.9 sawa
na asilimia 105 ya lengo tulilopangiwa na Serikali,”amesema Shija.
Amesema kuwa mwaka
ujao wa fedha 2025/2026 wameongezewa lengo kwa kupangiwa kukusanya Shilingi
Bilioni 10.5 na mategemeo yao kwa mwenendo uliopo wa ukuaji wa sekta ndani ya
mkoa watafanikiwa kulifikia lengo hilo.
0 Maoni