Kukamilika kwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Seronera
(Seronera Airstrip) uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti umeelezwa kuwa
kichocheo muhimu cha ongezeko la idadi ya watalii nchini Tanzania.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hassan
Abbasi ameeleza kuwa kukamilika kwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Seronera
(Seronera Airstrip) uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti utachochea
ongezeko la watalii wa ndani na nje.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo jana Mei 9, 2025 wakati akifanya
ukaguzi wa miundombinu ya utalii iliyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Aidha, Dkt. Abbasi alielekeza usimamizi wa uwanja huo baada
ya kupokea maelezo ya kukamilika kwa ukarabati wa uwanja ambapo matengenezo
yaliyofanyika ni pamoja na upanuzi wa eneo la uwanja lijulikanalo kana
“Taxway”, njia ya ndege yenye urefu wa mita 15 pamoja na upanuzi wa sehemu ya
kutua ndege (runway) yenye urefu wa Kilomita 2.3 na upana wa mita 30.
Ziara ya Dkt. Abbasi ni mwendelezo wa ziara ya ukaguzi
wa miradi ya maendeleo ndani ya Hifadhi
ya Taifa Serengeti ambapo awali alitembelea na kukagua maeneo ya uwekezaji wa
malazi katika hoteli ya Serengeti Explorer na Serengeti Lake Magadi Lodge
zilizopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Dkt. Abbasi amewaalika wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii ikiwemo malazi katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, hifadhi nyingine za Taifa pamoja na maeneo mengine yaliyohifadhiwa ili kuendelea kuunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuhakikisha kuwa Tanzania inapokea idadi kubwa ya watalii na mapato yatokanayo na utalii.
0 Maoni